Home » » Baba aua bintiye kwa panga

Baba aua bintiye kwa panga



MKAZI wa Tengerea, wilayani Mkuranga, Pwani, Hassan Mohammed (42) maarufu kwa jina la Nailoni, anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kumuua binti yake kwa kumkata kwa panga.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Ulrich Matei alisema tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Septemba 20  mwaka huu katika Kijiji cha Tengerea, ambako Mohammed alimuua bintiye, Amina Hassan (17) kwa kumkata panga shingoni na kichwani.
Kamanda Matei alieleza uchunguzi wa awali umebaini mtuhumiwa huyo ana maradhi ya akili. Mwili wa marehemu umehifadhiwa Hospitali ya Wilaya ya Mkuranga kwa uchunguzi.
Katika tukio lingine, Hamisi Maliki, mkazi wa Hoyoyo ameuawa na wananchi baada ya kutuhumiwa kuvunja duka la Edward Mikael, katika Kijiji cha Mivule Wilaya ya Mkuranga.
Katika tukio la tatu, mtu mmoja amefariki dunia na mwingine kujeruhiwa baada ya gari T 748 ADX Scania kupasuka tairi la nyuma kulia na kupinduka katika Kijiji cha Msolwa Wilaya ya Bagamoyo.
Kamanda Matei alimtaja aliyefariki dunia kuwa ni Marid Mtamwa, mkazi wa Njombe na majeruhi ni Erick Mvula, utingo wa gari hilo ambaye amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Tumbi.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Pwani Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa