BAADHI ya wamiliki wa vituo vya
kulelea watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu wametahadharishwa
kuacha tabia ya kuchagua watu,makundi na taasisi za kuwapelekea misaada
mbalimbali kwani kwa kufanya hivyo wanawanyima fursa watoto waliopo vituoni
humo kupata misaada na hata nafasi ya kukaa na kubadilishana mawazo.
Tahadhari hiyo imetolewa jana
wilayani Kibaha na wanakikundi wa kikundi cha Ebeneza cha Dar esalaam wakati
wakitoa misaada mbalimbali ya vyakula,vinywaji,nguo na viatu kwa watoto yatima
na wanaoishi katika mazingira magumu wanaolelewa kwenye kituo cha Buloma
Foundation wilayani humo mkoani Pwani.
Akizungumza baada ya kukabidhi
msaada huo,mwenyekiti wa Ebeneza David Stephen amesema msaada ni kama zawadi
kwa watoto hivyo siku sote anayepewa si lazima alazimishe jamii impe nini na
badala yake anatakiwa kueleza changamoto alizonazo na kisha kusubiri atasaidiwa
kipi kati ya alizozitaja.
Stephen amesema kikundi hicho
kimefikia hatu ya kutoa rai kwa wamiliki wa vituo vya kulelea watoto yatima
baada ya wao kukumbana na changamoto katika baadhi ya vituo walivyopanga awali
kuvitembelea na kutoa msaada wa vitu mbalimbali ambapo wao walitakiwa kupeleka
tofauti na walivyojiandaa.
Misaada iliyotolewa na Ebeneza
kituoni hapo ni pamoja na sembe,mchele,maharage,ngano na sukari kila mmoja kilo
50,nguo na viatu vya watoto aina na saizi mbalimbali,mafuta ya
kupaka,madaftari,juisi,lishe,sabuni za kufulia,mafuta ya kupikia,chumvi,dawa ya
mswaki,biskuti vyote vikiwa na thamani ya sh.milioni moja fedha ambazo zimetoka
katika mfuko wa kikundi hicho chenye lengo la kusaidiana wenyewe na jamii ya
mahitaji maalumu.
Awali mmiliki wa kituo hicho cha
Buloma Ana Kyando amesema kwa sasa anahudumia watoto wenye mahitaji maalumu 30
wa umri wa miaka miwili hadi 15 na kati wao wasichana ni 14 na kwamba
wamegawanyika kwenye makundi matatu ya waliopatikana baada ya kutupwa vichakani
na wazazi wao,waliotelekezwa sehemu mbalimbali kama gesti pamoja na kundi la
yatima na mazingira magumu.
Mama Kyando amewashukuru
wanakikundi hao kujitolea fedha zao za mifukoni na kuwasaidia watoto na kuitaka
jamii kutambua kuwa jukumu la kuwatunza yatima na waishio mazingira magumu ni
la kila mmoja na siyo kutegemea Serikali pekee.
0 comments:
Post a Comment