na Julieth Mkireri, Kibaha
MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Taifa
(NEC) kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kibaha Mjini, Rugemalila
Rutatina, ameiomba serikali ya Mkoa wa Pwani kufungua barabara za ndani ili
kuwezesha wafanyabiashara kusafirisha bidhaa kwa urahisi.
Rutatina alitoa ombi hilo mwishoni
mwa wiki alipozungumza na waandishi wa habari na kusema ni vema serikali ya
mkoa ikafanya jitihada za kufungua barabara hizo ambazo hutumiwa na wafanyabiashara
wengi wakiwamo vijana ambao wanajishughulisha na shughuli za ujasiriamali, ili
waweze kusafirisha mazao yao bila usumbufu.
Aidha, alisema kuwa suala la ajira
kwa vijana ndani ya taifa bado ni tatizo kubwa ingawa serikali inaendelea
kuweka mikakati ya kuhakikisha tatizo hilo linakomeshwa, hivyo ni jambo jema
endapo barabara zilizopo ndani ya mikoa zinazounganisha wilaya zitafunguliwa
ili zisaidie wakulima na wajasiriamali vijana kusafirisha bidhaa zao kwa
urahisi..
Alisema ili kufikia lengo la kutoa ajira kwa
vijana ni vema serikali ikafungua barabara zinazounganisha wilaya zake kama
vile Bagamoyo -Kibaha, Kisarawe - Mkuranga na nyinginezo ambazo zitawasaidia
wananchi hususan wakulima kupata unafuu wa masoko.
CHANZO TANZANIA DAIMA
0 comments:
Post a Comment