na Victor Masangu, Pwani
JAMII imetakiwa
kuachana na dhana potofu ya kuwabagua na kuwadharau watu wenye ulemavu wa
kutosikia na badala yake wawashirikishe katika shuguli mbalimbali za
kimaendeleo pamoja na kuwapatia fursa katika nafasi za uongozi.
Kauli hiyo
ilitolewa jana na Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanawake Viziwi Tanzania (MWAVITA),
Happiness Thomas, alipokuwa akifungua warsha inayohusiana na utawala bora,
uwazi na uwajibikaji iliyofanyika wilayani Kibaha.
Alisema kundi
la watu wasiosikia limekuwa katika wakati mgumu kutokana na jamii kulinyanyasa
kwa kutolitendea haki za msingi na kulinyima fursa ya kushirikishwa katika
utekelezaji wa majukumu mbalimbali.
Alisema jamii
ya watu ambao hawana ulemavu inapaswa kuhakikisha inawashirikisha kikamilifu
watu wenye ulemavu wa kutosikia katika kila jambo ambalo linaweza kuleta
mabadiliko makubwa ya kimaendeleo.
“Kwa kweli sisi
kama walemavu wa kutosikia (viziwi) tumekuwa katika wakati mgumu sana na hii
yote ni kutokana na kubaguliwa na jamii ya watu wasio walemavu, hivyo tunaomba
watupe ushirikiano wa kutosha na kuhakikisha wanatushirikisha katika shughuli
mbalimbali za kimaendeleo,” alisema Happiness.
Aidha, alisema
watu wenye ulemavu wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwezo uhaba wa
wakalimani wa lugha za alama, kwani wakati mwingine wanapokwenda kushiriki
mikutano na vikao mbalimbali wanashindwa kuelewa mambo ya msingi
yanayozungumzwa.
Naye meneja wa
mradi wa mtandao huo, Aneth Gerana, alisema watu wenye ulemavu wana uwezo
mkubwa katika kutekelza majukumu mbalimbali ya kuleta chachu ya maendeleo,
hivyo serikali inapaswa kuhakikisha inawashirikisha katika nafasi mbalimbali za
uongozi kama ilivyo nchi nyingine.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment