Home » » Mbunge ahojiwa na Takukuru kwa rushwa

Mbunge ahojiwa na Takukuru kwa rushwa


Mwandishi Wetu, Kisarawe
MBUNGE wa Viti Maalumu (CCM), Mkoa wa Pwani Zaynab Vullu, amekamatwa na kutakiwa kutoa maelezo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) akituhumiwa kujihusisha na rushwa.Vullu alitiwa mbaroni juzi jioni katika Ofisi za CCM Wilaya ya Kisarawe akidaiwa kuendesha kikao ambacho kiliandamana na utoaji rushwa.
Habari zilieleza kuwa maofisa hao wa Takukuru walivamia kikao hicho kilichokuwa kikiongozwa na mbunge huyo ambaye ni Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Pwani na kuwachukua Vullu na viongozi wengine kadhaa wa Jumuiya hiyo kwa mahojiano.
Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Pwani, Joyce Shirima alithibitisha tukio hilo lakini akasema asingependa kuzungumzia suala hilo kwa kina kwa sababu bado linafanyiwa uchunguzi.“Ni kweli tukio hilo lipo lakini mimi kwa sasa sipo kwenye position nzuri (nafasi) ya kuongea isipokuwa uchunguzi bado unaendelea na nitatoa maelezo zaidi baadaye,” alisema Shirima.
Vullu alikiri tukio hilo na kueleza kuwa lilitokana na fedha ambazo zilikuwa zikigawiwa kwa wajumbe wa kikao hicho ambazo alisema kuwa ni posho halali kwa ajili ya safari na chakula cha mchana. Lakini akasisitiza kuwa haikuwa rushwa.

“Hawakutukamata, bali walitutaka twende katika Ofisi za Takukuru za Wilaya kwa ajili ya mahojiano,” alisema Vullu na kuwataja alioongozana nao kwenda katika ofisi hizo kuwa ni Katibu wa CCM Wilaya ya Kisarawe, Vena Mgaya,   Katibu wa UWT wa Wilaya, Mwajuma Mwombe, Mwenyekiti wa UWT wa Wilaya hiyo, Asia Madina na wajumbe wa kikao hicho.
“Utaratibu wa chama uko wazi, kama kuna kikao ni lazima kiandaliwe chakula kwa ajili ya wajumbe na kulipana posho, sasa hiyo huwezi kusema kuwa ni rushwa.”
Hata hivyo, Vullu alisema kuwa kila mtu alikwenda Takukuru kwa muda wake na walikaa huko kuanzia saa 10 jioni hadi saa 1:30 usiku, bila kuhojiwa.
“Wapo ambao waliitwa majina yao lakini hawakuwepo katika eneo hilo na sisi majina yetu hayakuitwa, tulianza kuhoji sababu za kuitwa kwa lengo la kuhojiwa,” alisema Vullu na kuongeza:
“Ilipofika usiku niliondoka kurudi nyumbani na hivi ninavyozungumza na wewe niko nyumbani na hakuna jambo lolote linaloendelea,” alisema Vullu.
Alisema maofisa hao wa Takururu walikamata fedha zilizokuwa zinatolewa kwa wajumbe na kusababisha baadhi yao kukosa nauli baada ya kikao hicho kuvunjika ghafla.
Alisema maofisa hao waliondoka na kitabu cha Kanuni na Katiba ya UWT, kitabu cha kumbukumbu (diary) mali ya katibu wa UWT kilichodaiwa kuwa na Sh50,000 na karatasi yenye majina ya wajumbe waliohudhuria katika kikao hicho.
“Sisi huwa tuna taratibu za kupeana posho kama bajeti ikiruhusu katika vikao vyote halali. Iwapo iliyokuwa inatolewa hapo ni rushwa basi hata chakula tulichokula ni rushwa na kama ile ilikuwa rushwa kweli mbona waliopokea hawajakamatwa?” alihoji Vullu.
Akizungumzia kukamatwa kwao, Asia ambaye pia ni Diwani wa Viti Maalumu Kisarawe alisema: “Tulikuwa tunatoa posho kwa wanajumuiya. Kila mwanajumuiya tulipanga apate Sh10,000 kama posho ambazo wengine zinawasaidia kwa nauli kutokana na wanachama kukaa mbali na ofisi za chama.”
Alisema wakati walipoingia maofisa hao walimkuta akiwa ameshikilia mkononi Sh550,000 ambazo walizichukua na kusababisha baadhi ya wajumbe kukosa.
Alidai kuwa ofisi yake ilipata fedha hizo kutokana na vyanzo mbalimbali, wakiwemo madiwani na wanasiasa wa CCM. Alisema michango hiyo iliwawezesha kupata Sh600,000 ambazo walizitenga kwa ajili hiyo.
Alisema wanachama 49 na mhudumu mmoja walikuwa kwenye orodha ya waliokuwa wapewe posho hizo na kusema kwamba taarifa kwamba alitoa rushwa zilisambazwa na wabaya wake baada ya kujua kuwa anaitetea nafasi yake ya uenyekiti wa UWT.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Pwani Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa