RAIS Jakaya Kiwete ameweka jiwe la msingi ujenzi wa barabara kuu ya Bagamoyo- Msata, mkoani Pwani huku akionyesha kusikitishwa na changamoto mbalimbali zinazotokana na matumizi mabaya ya barabara za lami zinazosababishwa na uzembe wa baadhi ya madereva nchini.
Barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 64, inayotarajiwa kuwa barabara kuu ya kupitisha mabasi na magari yote yatokayo na kwenda mikoa ya Kanda ya Kaskazini kutoka Dar es Salaam na inajengwa na Kampuni ya M/S Estim Contruction kwa Sh89.6 bilioni.
Kikwete ambaye aliwasili Kijiji cha Kiwangwa jana saa 5:50 asubuhi kwa helikopta ya polisi, alisema serikali imekuwa ikifanya jitihada za kuboresha miundombinu ya barabara sehemu mbalimbali nchini, lakini kikwazo kikubwa ni matumizi sahihi.
Alisema mwaka jana vifo vya watu 3,981 vilitokea kwa kusababishwa na ajali za barabara, huku 20,800 wakijeruhiwa.
Alishauri wenye mamlaka kuanzia ngazi za wilaya, mkoa na taifa kuangalia hali hiyo ili barabara hiyo kuu ya Bagamoyo- Msata ikishamalizika kila mtu azingatie matumizi ya barabara, kwani ni mojawapo ya miundombinu inayojengwa kwa gharama kubwa.
Awali, Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli alisema hadi sasa tayari kilomita 39 zimeshajengwa kwa lami na kwamba, mradi huo wote utagharimu Sh95 bilioni, huku Sh89.6 bilioni zikiwa na mjenzi, Sh1.47 bilioni msimamizi na Sh3.9 bilioni za kulipa fidia.
Dk Magufuli alisema fedha za mradi huo zinatolewa na Serikali ya Tanzania na kwamba, uwapo wa barabari hiyo ni mkombozi kwa wakazi wa Bagamoyo na Tanzania.
Pia, Dk Magufuli alimuomba Rais Kiwete kupitia kwa viongozi wa makandarasi nchini kuwajibisha Kampuni ya M Consultant na ikiwezekana ifutiwe leseni ya kufanya kazi nchini na Afrika Mashriki, ili iwe fundisho kwa sababu imeingizia serikali hasara baada ya kufanya makadirio ya chini ya kiwango ujenzi wa barabara hiyo.
Habari na Julieth Ngarabali, Pwani
Chanzo - Mwananchi
0 comments:
Post a Comment