KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeunga mkono
uamuzi uliofikiwa na kamati maalumu iliyoundwa na serikali kwa ajili ya
kutafuta suluhu ya kumaliza mgogoro wa ardhi baina ya Hifadhi ya Taifa
ya Saadani na wananchi wa kitongoji cha Uvinje walioanzisha makazi ya
kudumu ndani ya hifadhi kinyume cha sheria.
Kamati hiyo iliyoundwa na wajumbe watatu ambao ni Serikali ya Wilaya
ya Bagamoyo, uongozi wa Kitongoji cha Uvinje na Mamlaka ya Hifadhi za
Taifa (TANAPA) kupitia Hifadhi ya Saadani, ilifikia maazimio kuwwananchi
wa kitongoji hicho walioanzisha makazi ndani hifadhi waondolewe kwa
kulipwa fidia ili kumaliza mgogoro huo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana wilayani Bagamoyo, Mwenyekii
wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Ardhi, Maliasili na Utalii, Atashasta
Ndetiye (pichani) alisema baada ya kutembelea eneo hilo, wamejiridhisha
kuwa kitongoji hicho cha Uvinje kimeanzishwa ndani ya eneo la hifadhi
ambapo ni kinyume cha sheria.
“Kiuhalisia tumeona kuna kitongoji ndani ya Hifadhi ya Taifa ya
Saadani, tumewasikiliza wananchi, tumesikiliza upande wa serikali, kwa
mujibu wa taratibu na sheria wale wananchi wanapaswa watoe ushirikiano,
tunaamini kuna taratibu za kiserikali zinafanywa kuhakikisha wale
wananchi wanalipwa ili waondoke kwa usalama,” alieleza Ndetiye.
Aliongeza, “tumeona jinsi ambavyo baadhi ya wananchi hawako tayari
kulipwa, lakini nadhani wakieleweshwa vizuri wataelewa kuwa ile ni
hifadhi ya Taifa, na kama ni hifadhi ya Taifa basi inahusu maslahi ya
Taifa, hivyo kila mwananchi anatakiwa atoe ushirikiano ili angalau
serikali ifanye uwekezaji wa kueleweka.”
Ndetiye alisema kamati hiyo imeshaweka maazimio kwa ajili ya
kulishauri Bunge ili liazimie ni nini kifanywe na serikali kumaliza
mgogoro huo. Alisema, “Kwa udharura wake na kutokana na maelezo ya mkuu
wa wilaya, kwa ujumla kamati inakubaliana nayo kwa sababu ameeleza vitu
ambavyo tumeona vina tija zaidi kwa Watanzania na tunaenda kulishauri
Bunge na serikali haraka iwezekanavyo ili hatua ziweze kuchukuliwa.”
Awali akielezea kuhusu mgogoro huo, Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Majid
Mwanga alisema baada ya maazimio ya kamati iliyoundwa na Serikali ya
Wilaya kumaliza mgogoro huo, baadhi ya wananchi walikubali maazimio
yaliyowekwa ya kulipwa fidia huku wengine wakikaidi kuondoka akiwemo
mwekezaji aliyeshikilia sehemu ya eneo hilo kwa zaidi ya miaka tisa bila
kuwekeza mradi uliokusudiwa ambao wamepewa kipindi cha mwezi mmoja
waondoke kwa hiari kabla ya nguvu kutumika kuwaondoa.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Uvinje, Hussein Akida alisema kitongoji
hicho kilianzishwa ndani ya Kijiji cha Saadani katika Wilaya ya Bagamoyo
mkoani Pwani zaidi ya miaka 100 iliyopita huku kikiwa na ukubwa hekta
3,000 na mpaka sasa kina kitongoji hicho kina wakazi wasiopungua 70.
Aliiomba serikali kutambua mipaka ya kitongoji hicho pamoja na
kuwasogezea wananchi huduma za kijamii. Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii walitilia shaka uwiano wa
kimahesabu wa taarifa hiyo na uhalisia, na kuhoji iweje kitongoji chenye
miaka mingi kiasi hicho kiwe bado hakijapewa hati ya kuwa kijiji kamili
pamoja na idadi ndogo ya wananchi wasiongezeka ndani ya muda mrefu wa
miaka zaidi ya 100 tangu kuanzishwa kwa kitongoji hicho.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Ramo Makani
alisema mgogoro huo uko wazi na unapaswa kumalizika mara moja kwa kuwa
Serikali ya Wilaya kupitia kamati iliyoundwa imeshafikia maazimio ya
kuwaondoa wananchi walioanzisha makazi ndani ya eneo la hifadhi kinyume
cha sheria. Alitoa mwito kwa wananchi kutii sheria za hifadhi na
kuheshimu mipaka iliyowekwa kuepusha migogoro isiyo ya lazima baina ya
serikali na wananchi.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment