Home » » WATOTO KUPATA KITUO

WATOTO KUPATA KITUO

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.


Askofu wa KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dk. Alex Malasusa.
KANISA la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Mashariki na Pwani, linatarajia kuanza ujenzi wa kituo cha watoto wenye ulemavu katika eneo la Mlandizi mkoani Pwani kitakachotoa mafunzo ya ufundi.

Ujenzi huo unatarajiwa kugharimu Sh. bilioni 6 fedha ambazo zitatokana na harambee kutoka kwa waumini wa kanisa hilo na wafadhili kitahudumia watoto 500.

Askofu wa KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dk. Alex Malasusa, aliyasema hayo juzi kwenye maonyesho ya kazi zinazofanywa na watoto wenye ulemavu Usharika wa Mtoni, jijini Dar es Salaam.

Dk. Malasusa, ambaye ni Mkuu mstaafu wa Kanisa hilo nchini, alisema watoto wenye ulemavu wanahitaji upendo na kusomeshwa na kuwaonya baadhi ya watu katika jamii wanaodhani watoto hao ni laana na kuamua kuwafungia ndani.
“Tofauti ya binadamu mmoja na mwingine, waliozaliwa na ulemavu na waliozaliwa wakiwa timilifu, inatukumbusha na kutujenga kiimani, Mungu ana makusudi yake, hivyo tuwahudumie,” alisema Dk. Malasusa.

Alieleza kwamba jamii ina wajibu wa kuwapa haki ya elimu watoto hao ambayo itawafanya wapate faraja.

Mratibu Kituo cha kulea watoto Usharika wa Mtoni, Dorice Mbuya, alisema changamoto iliyopo kituoni hapo ni uhaba wa majengo, zikiwamo ofisi na madarasa.

Alisema kituo hicho kina watoto 49 na kwamba kuna maombi ya watoto 70 wanaotakiwa kujiunga, lakini wameshindwa kujiunga kutokana na uhaba wa majengo.

“Watoto 70 wanasubiri mradi wa ujenzi wa majengo mapya na kukarabati mengine ambayo yatatosheleza idadi yao,” alisema Mbuya.

Alisema kituo kinatoa huduma tofauti, ikiwamo elimu ya ufundi, ujasiriamali na kuwapima kiafya watoto wenye matatizo ya afya ya akili.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Pwani Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa