Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo
MKUU wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo ameagiza ifikapo leo,
wakurugenzi wa halmashauri za mkoa huo, wawe wamewapa zawadi zao
watumishi bora wa mwaka huu baada ya kubaini walitoa zawadi hewa kwenye
sherehe za Mei Mosi.
Ameagiza pia Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa wa Pwani pamoja na
mkurugenzi wa Shirika la Elimu Kibaha, nao kutoa zawadi ya fedha kwa
wafanyakazi waliofanya vizuri kwenye vitengo vyao, badala ya kuwapa
vyeti pekee.
Akizungumza juzi kwenye sherehe za Mei Mosi zilizofanyika kimkoa
wilayani Mkuranga, Ndikilo alitoa siku tatu zinazoisha leo, taasisi hizo
ziwe zimetekeleza agizo hilo. Alisema walichofanya ni masihara na yeye
hayuko tayari kufanyiwa mzaha katika suala hilo, lililoandaliwa kwa muda
mrefu.
“Katika risala ya Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi Tanzania
(TUCTA) Mkoa wa Pwani walilalamika kuwa kumekuwa na tabia ya baadhi ya
waajiri kuwakopa zawadi za fedha watumishi wanaofanya vizuri kama
motisha,” alisema.
Aliendelea, “Lakini kwa hali hii siwezi kukubaliana nalo, nawapa siku
tatu muwe mmewalipa watumishi hao vinginevyo atakayeshindwa aje ofisini
kwangu akutane na adhabu niliyoiandaa.”
Alisema hawezi kuvumilia watu wazembe wanaofanya dharau kwenye mambo
mazito na kwamba atachukua hatua kali kwa halmashauri ambazo zitashindwa
kutoa zawadi hizo kwani zingine zimetoa kwa nini wengine washindwe.
“Mimi siyo mtani wenu, wala si saizi yenu, haiwezekani mniite nije
kutoa zawadi hewa, ndo maana hatua zikichukuliwa za kinidhamu mnasema
mnaonewa, ikifika Jumatano muwe mmeshawapa zawadi zao wahusika, huu ni
mzaha umepitiliza kiwango anayedhani tunatania aendelee aone,” alisema
Ndikilo.
Licha ya ofisi ya Katibu Tawala pamoja na Shirika la Elimu Kibaha,
taasisi nyingine zilizotakiwa kutekeleza agizo ni Halmashauri ya Wilaya
ya Bagamoyo, Halmashauri ya Mji Kibaha na Halmashauri ya Wilaya ya
Rufiji .
“Hatutaniani hapa huu ni mzaha uliopitiliza kiwango ujumbe umefika
namna hii mnakatisha tamaa watumishi kwa kudai kuwa mchakato bado ni
jambo ambalo halijanifurahisha na nisingependa hali hii isijitokeze
tena,” alisema Ndikilo.
Awali, akisoma risala ya Tucta, Amini Msambwa alisema kuwa
wafanyakazi wana haki ya kutimiziwa haki zao za msingi na siyo lazima
zipatikane kwa shinikizo la maandamano, migomo na hata kufungia nje
waajiri.
Msambwa alisema kuwa moja ya changamoto ni baadhi ya wawekezaji wa
nje na wa ndani, kuwanyima fursa wafanyakazi kujiunga na vyama vyao
sehemu za kazi, ambayo ni haki yao ya kisheria na kwa kuzingatia kauli
mbiu ya mwaka huu ya Dhana ya Mabadiliko ilenge kuinua hali za
wafanyakazi.
Chanzo Gazeti la Habari leo
0 comments:
Post a Comment