Meneja Uhusiano wa Jamii wa
Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es salaam (DAWASA) Bi.Neli Msuya
akizungumza na viongozi wa Jumuiya 15 za Watumia Maji zilizojengwa chini ya
mradi wa Maji Yetu uliofadhiliwa na Serikali ya Ubelgiji uliogharimu shilingi
Bilioni 14.5 alipokutana nao leo jijini Dar es salaam.
Mshauri wa Ufundi wa DAWASA
–BTC Mhandisi Praygod Mawalla akitoa elimu kwa
viongozi wa Jumuiya 15 za Watumia Maji katika jiji la Dar es salaam namna ya
kuifanya miradi wanayoisimamia ijiendeshe na kuwa endelevu kwa manufaa ya
wananchi.
Mshauri wa Ufundi wa DAWASA –BTC Manjolo Kambili
akitoa akitoa ufafanuzi kuhusu Programu ya za utoaji wa mafunzo kwa watumiaji
wa Maji katika maeneo yenye miradi hiyo wakati wa mkutano na viongozi wa
Jumuiya 15 za Watumia Maji za jiji la Dar es salaam.
Viongozi wa Jumuiya 15 za
Watumia Maji zilizojengwa chini ya mradi wa Maji Yetu wakifuatilia mada mbalimbali zilizokuwa zikiwasilishwa na watendaji
wa DAWASA leo jijini Dar es salaam.
Afisa Uhusiano na Jamii wa Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es
salaam (DAWASA) Bi. Mecktridis Mdaku Mtaalamu
kutoka akiwasisitiza viongozi wa Jumuiya 15 za Watumia Maji katika
jiji la Dar es salaam kupanda miti na kuiendesha miradi katika hali ya Usafi
ili kulinda afya za watumiaji wa huduma za maji.
Mkurugenzi wa Rasilimali watu na Utawala wa DAWASA Bi. Mary Ntikula akipanda mti mara baada ya mkutano na viongozi wa Jumuiya ya Watumia Maji Dar es salaam kama sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Maji na Utunzaji wa Mazingira. Kulia ni Meneja Uhusiano wa Jamii wa
Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es salaam (DAWASA) Bi.Neli Msuya
Baadhi ya watendaji wa
Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es salaam (DAWASA) wakiwa katika picha ya
pamoja na Viongozi wa Jumuiya 15 za Watumia Maji jijini Dar es salaam.
Na. Aron Msigwa –Dar es salaam.
Mamlaka ya Maji Safi na Maji
Taka Dar es salaam (DAWASA) imewataka viongozi wa Jumuiya za watumia maji
katika jiji la Dar es salaam na baadhi
ya maeneo ya Kibaha na Bagamoyo mkoani Pwani kusimamia kikamilifu mapato na
matumizi ya miradi ya maji ili kuepuka migogoro inayosababishwa na matumizi
mabaya ya fedha jambo linalochangia baadhi ya miradi kushindwa kujiendesha na
kuwa kero kwa wananchi.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini
Dar es salaam na Meneja Uhusiano wa Jamii wa Mamlaka hiyo Bi.Neli Msuya wakati
akitoa elimu kwa viongozi hao kuhusu uendelezaji wa miradi inayosimamiwa na Jumuiya
15 za Watumia Maji zilizojengwa chini ya mradi wa Maji Yetu kwa ufadhili wa
Serikali ya Ubelgiji.
Amesema DAWASA imekukutana viongozi hao kuwakumbusha wajibu walio nao
katika kuhakikisha miradi wanayoisimamia inakidhi matarajio ya wananchi kwa kutoa
huduma bora na kujiendesha kwa faida kwa na kuwafikia wananchi wengi zaidi.
“Kwa kuzingatia idadi ya watu zaidi ya Laki mbili (200,000) wanaohudumiwa na mradi huu kwa kupata maji
safi na salama na gharama kubwa iliyotumika kuanzisha mradi huu shilingi
Bilioni 14.5 ,tumeona kuna umuhimu wa kuendelea kuweka msisitizo wa uangalizi kwa
kuwa miradi hii ni muhimu na iko kwa wananchi” Amesisitiza.
Amewaeleza viongozi hao kuwa majukumu ya DAWASA
kama mmiliki wa miundombinu ya majisafi na majitaka ni kugharamia matengenezo
makubwa na kufanya uwekezaji wa kupanua miundombinu ya majisafi na majitaka
jijini Dar es Salaam na maeneo yaliyoainishwa chini ya Sheria ya DAWASA
Namba.20 ya Mwaka 2001.
Bi. Neli amefafanua kuwa DAWASA iliingia mkataba
wa uendeshaji na Shirika la Majisafi na Majitaka Dar es salaam (DAWASCO) kutoa
huduma ya uondoshaji wa majitaka katikA jiji la Dar es salaam, Kibaha na
Bagamoyo mkoani Pwani.
Aidha, amesema kupitia mkataba huo, DAWASCO huuza maji kwa wateja, kutayarisha Ankara
za maji, kukusanya maduhuli, kulipia gharama za uendeshaji na kufanya
matengenezo ya mfumo mzima wa usambazaji maji na uondoshaji majitaka katika
maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es salaam.
“Kupitia
elimu inayotolewa leo mtagundua kuwa ninyi ni muhimu katika kuwahudumia wananchi,
mtaona kuwa ninyi ni DAWASCO ndogondogo kwenye maeneo yenu kwa kuwa mnauza maji
kwa wateja, mnatayarisha Ankara za maji , mnakusanya fedha za malipo ya huduma mnafanya
matengenezo ya mifumo ya maji kwa wateja wenu” Amesisitiza.
Amesema kwa sasa DAWASA imewekeza kwenye miradi
mikubwa na kupanua chanzo cha Maji cha Ruvu chini ambacho huzalisha lita
milioni 270 kwa siku, ujenzi wa Bomba kubwa lenye urefu wa Kilometa 56 kutoka
Ruvu Chini hadi matenki yaliyopo chuo Kikuu Ardhi jijini Dar es salaam.
Aidha amesema kwa upande wa Ruvu juu maboresho
makubwa yamefanyika kwa kupanua mitambo ya uzalishaji ambayo sasa itazalisha lita
milioni 196 kutoka milioni 82 kwa siku.
Ameongeza kuwa upande wa maeneo ya kaskazini na
kusini mwa jiji la Dar es salaam kuelekea wilaya ya Mkuranga DAWASA inaendelea
kuwekeza katika uchimbaji wa visima virefu vya maji na kuweka mifumo ya
usambazaji wa maji ili kuwawezesha wananchi kupata maji safi na salama kwa
gharama nafuu.
Kwa upande wake Mshauri wa Miradi ya Maji kutoka
DAWASA –BTC Bw. Manjolo
Kambili amewaeleza viongozi hao kuwa wao kama viongozi wa Jumuiya za watumia
maji wanatakiwa kufuata sheria na taratibu za Serikali kwa kuwa miradi hiyo ni
ya Serikali.
Ameeleza kuwa jukumu la kusimamia na miradi hiyo
liko kisheria hivyo viongozi hao wanapaswa kutekeleza kikamilifu majukumu yao
likiwemo la kuhakikisha kuwa miradi yote inaajiri wahasibu wenye taaluma kwa
lengo la kuandika na kutunza kumbukumbu za kila siku zinazohusu mapato na
matumizi yao.
“Naomba nisisitize katika hili, nyie mmepewa
jukumu la kusimamia miradi ya maji ya Serikali, lazima mlitambue hili miradi
yenu itakaguliwa na wataalamu ndio maana tuliwaomba muajiri wahasibu kwa kuwa
vitabu vyenu vitakaguliwa kujua mwenendo wa mapato na matumizi yenu” Amesisitiza.
Amewataka viongozi hao kuhakikisha kuwa kila mradi
wa jumuiya unakuwa na akaunti ya Benki pamoja na kusimamia suala la utoaji wa
risiti halali zenye nembo za jumuiya husika ili kuweka uwazi na imani wa
walipiaji Ankara za maji.
Naye Afisa Uhusiano na Jamii wa Mamlaka hiyo Bi.
Mecktridis Mdaku amewasisitiza viongozi hao kusimamia suala la Usafi wa
mazingira, upandaji wa miti na utunzaji wa vituo vya miradi, majengo na miundombinu ya
maji ili kuwakinga wananchi dhidi ya magonjwa ya milipuko ikiwemo.
“Ninyi kama viongozi wa Kamati za miradi ya maji
lazima msimamie suala la usafi wa mazingira ili maeneo ya miradi yavutie pia
kuwakinga wateja wenu na ugonjwa wa kipindupindu” Amesisitiza Bi. Mdaku.
Ametoa wito kwa viongozi hao kuepuka kuyatumia
majengo ya miradi ya maji ya wananchi kwa shughuli nyingine nje ya maji ikiwemo kuhifadhi na kufanyia
biashara ya mkaa.
MWISHO.
0 comments:
Post a Comment