Home » » Mama Salma Kikwete awataka Wanachama wa vikundi vya kukopa na kuweka akiba kuwa na uthubutu na kujiwekea malengo ya maendeleo kutokana na fedha wanazokopa‏

Mama Salma Kikwete awataka Wanachama wa vikundi vya kukopa na kuweka akiba kuwa na uthubutu na kujiwekea malengo ya maendeleo kutokana na fedha wanazokopa‏


 Mkuu wa Mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo akimkaribisha Mke wa Rais na Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo, WAMA, Mama Salma Kikwete mara baada ya kuwasili kwenye eneo la Shule ya Sekondari Zimbwini huko Kibiti, wilayani Rufiji, kuhudhuria sherehe za kutimiza mwaka za vikundi vya WAMA katika mradi wa Mwanamke Mwezeshe tarehe 7.3.2015.
 Mwenyekiti wa WAMA na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akisalimiana na Ndugu Alife Omar Mtulia, Mwenyekiti wa Umoja wa Vikundi vya Mradi wa Mwanamke Mwezeshe wa Wilaya ya Rufiji wakati alipowasili kwenye uwanja wa Shule ya Sekondari Zimbwini zilikofanyika sherehe ya kutimiza mwaka kwa vikundi hivyo tarehe 7.3.2015.

 Mke wa Rais na Mwenyekiti wa WAMA, Mama Salma Kikwete akisalimiana na mmoja wa Maafisa watendaji wa Mradi wa Mwanamke Mwezeshe katika Wilaya ya Rufiji mara baada ya kuwasili huko Kibiti kuhudhuria sherehe za kutimiza mwaka za vikundi hivyo tarehe 7.3.2015.
 Baadhi ya akina mama wa Vikundi vya Mwanamke Mwezeshe wa Wilaya ya Rufiji wakiimba nyimbo za mafanikio ya vikundi vyao wakati wa sherehe za kutimiza mwaka huko Kibiti, wilayani Rufiji tarehe 7.3.2015.
 Wanachama wa Vikundi vya Mwanamke Mwezeshe wa Wilaya ya Rufiji wakiserebuka wakati wa sherehe za kutimiza mwaka kwa vikundi vyao zilizofanyika kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari Zimbwini huko Kibiti wilayani Rufiji katika Mkoa wa Pwani tarehe 7.3.2015.

 Mamia ya wana vikundi vya WAMA katika Mradi wa Mwanamke Mwezeshe katika Wilaya ya Rufiji wanaonekana wakisikiliza hotuba ya mgeni rasmi Mama Salma Kikwete, Mke wa Rais na Mwenyekiti wa Taasisi ya WAMA wakati wa sherehe za kutimiza mwaka kwa vikundi hivyo. Sherehe hizo zilifanyika huko Kibiti na kuhudhuriwa na wananchi na viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Pwani.

 Mke wa Rais na Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo,WAMA, Mama Salma Kikwete akiwahutubia mamia ya wana vikundi vya Mwanamke Mwezeshe na wananchi wa  Wilaya ya Rufiji wakati wa sherehe za kutimiza mwaka kwa vikundi hivyo zilizofanyika huko Kibiti tarehe 7.3.2015.
 Mke wa Rais na Mwenyekiti wa WAMA, Mama Salma Kikwete akimkabidhi cheti Afisa Mtendaji wa vikundi vya WAMA katika Mradi wa Mwanamke Mwezeshe Bibi Rehema Kipengele kwa kutambua uwezo wake mkubwa wa kuunda vikundi vingi zaidi hivyo kuvuka lengo alilopangiwa.
 Mke wa Rais na Mwenyekiti wa Taasisi ya WAMA, Mama Salma Kikwete akimkabidhi cheti cha Uvumilivu katika Mazingira Magumu ya kazi Bi Catherine Mfinanga, miongoni wa Maafisa Watendaji wa Mradi wa Mwanamke Mwezeshe katika Wilaya ya Rufiji katika sherehe zilizofanyika huko Kibiti tarehe 7.3.2015.

  Mwenyekiti wa WAMA na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akiangalia bidhaa mbalimbali zinazozalishwa na wana vikundi vya WAMA katka Mradi wa Mwanamke Mwezeshe katika Wilaya ya Rufiji wakati wa sherehe za kutimiza mwaka kwa vikundi hivyo zilizofanyika huko Kibiti tarehe 7.3.2015.



PICHA NA JOHN  LUKUWI. 


Na Anna Nkinda – Maelezo, Rufiji
 Wanachama wa vikundi  vya  kukopa na kuweka akiba wametakiwa kuwa na uthubutu na kujiwekea malengo ya maendeleo kutokana na fedha wanazokopa kwa kufanya hivyo wataweza kujikwamua kutoka maisha ya umaskini na kuongeza kipato cha familia.

Rai hiyo imetolewa na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati wa sherehe za kuadhimisha mwaka mmoja wa kuanzishwa kwa vikundi vya mradi wa Mwanamke Mwezeshe unaoongozwa na Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) zilizofanyika katika viwanja vya shule ya Sekondari ya  Zimbwini  iliyopo Kibiti wilayani Rufiji mkoa wa Pwani.

Mama Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa Taasisi hiyo alisema kupitia vikundi hivyo vya hisa wanawake wameweza  kukopa na kuweka akiba na kufanya mambo ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kulipa ada za watoto, kununua mashamba , viwanja, kujenga nyumba na hivyo kuongeza thamani yao katika jamii  kwani mwanamke akiwa na fedha mkononi hadhi  yake inaongezeka lakini akiwa ombaomba hadhi yake inapungua na kudharaulika na mme wake.

“Pamoja na jina la mradi huu kuitwa mwanamke mwezeshe nawasihi wanaume msiogope kujiunga kwani lengo la mradi ni kumkomboa mtanzania kutoka maisha ya umaskini pia vikundi vilivyopo katika mfumo huu vimeweza kupata huduma ya bima ya afya kupitia mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) hali kadhalika kupitia vikundi wanachama ameweza kupewa mafunzo ya kuwaongezea ujuzi kupitia semina na maonesho”.

Muwe makini na waaminifu kwani vikundi hivi ni nyenzo muhimu ya kuwakomboa. Msikubli kuondolewa katika lengo lenu la msingi la kuinua hali zenu za maisha na kutumiwa na watu wabaya kufanya mambo yaliyo kinyume, mkumbuke amani ya nchi ikipotea waathirika wakubwa ni kina mama na watoto”, alisema Mama Kikwete.

Aidha Mwenyekiti huyo wa Taasisi ya WAMA alisema huu ni mwaka wa uchaguzi mkuu na kupiga kura ya maoni na kuwataka  wanavikundi hao kuhakikisha  wanajitokeza kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura ili waweze kushiriki katika zoezi la kura za maoni na kuchagua katiba inayopendekezwa na mwishoni mwa mwaka huu kuchagua rais, mbunge na diwani.

Mama Kikwete alisisitiza, “Nawasihi ndugu zangu msiwasikilize watu watakaowashawishi msijitokeze kujiandikisha au msiende kupiga kura ya maoni kuhusu katiba inayopendekezwa. Na baya zaidi msikubali kufanya mambo yanayoweza kuvuruga amani ya nchi, Historia inatufundisha kuwa kila palipoharibika amani walioteseka zaidi ni wanawake na watoto”. 

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Pwani Evarist Ndekilo aliishukuru Taasisi ya WAMA kwa kuwawezesha wanawake katika mkoa huo kwani hivi sasa wanaweza kutoa michango mbalimbali ya kifedha katika jamii zao bila ya kumtegemea mwanaume tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma.

Alisema kupitia wataalam waliopo katika ofisi za Halmashauri za mkoa huo wakiwemo maafisa maendeleo ya jamii watahakikisha wanavisaidia vikundi hivyo ili viwe endelevu.
“Wanachama wa vikundi hivi nawaomba mshikamane na kushirikiana  bila ya kufanya hivyo mradi huu hautakuwa endelevu WAMA wamewapa nyavu nendeni mkavue samaki, ipandeni hii mbegu mliyopewa iweze kustawi  zaidi na hivi vikundi viwe vya mfano ili waliopo nje nao wajiunge”, alisema Ndekilo.

Akisoma risara ya vikundi hivyo Arafa Ngwaya ambaye ni mwalimu wa vikundi vya hisa na Katibu wa Umoja Ikwiriri alisema umoja huo umeanzishwa na vikundi vya hisa vipatavyo 51 venye wanachama 1643 kati ya hao wanaume 268 na wanawake 1375 ambavyo vimemaliza mzunguko wa mwaka wa kwanza na kugawana  hisa ya  shilingi 492,422,947/=.

Alisema madhumuni ya umoja huo ni kuviunganisha vikundi vya hisa wilaya ya Rufiji ili umoja uweze kusimama na kuleta ufanisi ikiwa ni pamoja na kutoa elimu ya ujasiriamali na ya utunzaji wa kumbukumbu za fedha kwa wanachama wake na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili katika biashara zao.

Kutafuta vyanzo mbalimbali vya mapato ikiwemo michango ya wanavikundi na wanahisa na mikopo kutoka taasisi mbalimbali za kifedha ili kuweza kuvikopesha vikundi vya wanachama.

“Changamoto zinazotukabili ni hakuna vifa vya kutosha vya kuendesha ofisi vifaa hivyo ni samani za ofisi na Computer, tunahitaji msaada wa kitaalam ili tuweze kufungua benki yetu kwani tunahakika malengo yetu yakitimia na changamoto hizi kutatuliwa tutakuwa tumepunguza suala la umaskini kwa kiasi kikubwa kama si kuondoa kabisa katika wilaya yetu”, alisema Arafa.

Akiongea jinsi alivyoweza kunufaika na mradi huo  Fatuma Mbuzi ambaye ni mkazi wa Ikwiriri anasema aliweka akiba na kukopa  fedha za mkopo wa kwanza ambazo alizitumia katika mradi wa  kutengeneza batiki, mkopo wa pili alinunua kiwanja na baada ya kumaliza mzunguko wa mwaka waligawana   hisa na kununua shamba.

Mradi wa Mwanamke Mwezeshe ulianza kufanya shughuli za kijamii mwanzoni mwa mwaka jana katika wilaya za Rufiji, Kilwa, Liwale, Lindi vijijini, Nachingwea kwa ufadhili wa Financial Sector Deeping Trust (FSDT) unalenga kuanzisha vikundi 3000 vyenye jumla ya wanavikundi 60,000 kwa kipindi cha miaka mitatu.

Hadi kufikia mwishoni mwa mwaka jana mradi ulikwishaunda vikundi 1,047 na kuwafikia wanavikundi 26,710 kati ya hivyo vikundi 450 viko wilaya ya Rufiji na vina wanavikundi 10,499. Mradi huo pia umetoa mafunzo ya kuweka akiba ambayo yatawawezesha wanavikundi kuweka akiba za jumla ya shilingi bilioni moja na nusu,  kufikia mwishoni mwa mwaka jana mradi ulikusanya shilingi 1,518,643,430/= na hivyo kuvuka lengo la mwaka la kukusanya akiba ya shilingi milioni 500.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Pwani Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa