Home » » TBS YAFUNGA KIWANDA CHA CHUMVI BAGAMOYO

TBS YAFUNGA KIWANDA CHA CHUMVI BAGAMOYO

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS), limekifunga kiwanda cha kuzalisha chumvi cha Sea Salt Company Limited, kilichopo Mjini Bagamoyo, eneo la Saadan, mkoani Pwani, kutokana na chumvi yake kutofaa kwa matumizi ya binadamu.

Kiwanda hicho kimefungwa juzi ambapo Ofisa Mdhibiti Ubora wa TBS, Deusdedith Paschal, alisema uamuzi huo unatokana na chumvi inayozalishwa kuwa na upungufu mkubwa wa madini joto yanayohitajika.

Alisema kiwanda hicho kitafunguliwa baada ya wahusika kufanya marekebisho na TBS kujiridhisha kwamba kinaweza kuendelea na uzalishaji.

Aliongeza kuwa, chumvi inatakiwa kuwa na kiwango cha madini joto miligramu 30-60, lakini chumvi ya Sea ina madini joto ya miligramu 14.9, jambo ambalo ni hatari kwa afya za watumiaji.

“Tumezuia kutolewa mifuko 276 ya chumvi iliyozalishwa ambayo ilikuwa tayari kwenda sokoni,” alisema Paschal na kuongeza kuwa, kiwanda hicho kiliomba kupatiwa leseni ya ubora TBS na baada ya shirika kufanya uchunguzi wa sampuri ya chumvi hiyo katika maabara zake wakabaini ina upungufu wa madini joto.

Paschal alisema mbali na chumvi hiyo kutokuwa na madini joto pia kipimo kinaonesha katika chumvi hiyo kuna vitu ambavyo haviwezi kuyeyuka kwenye maji.

“Kuna mchanga mwingi ambao ukiweka kwenye maji hauwezi kuyeyuka,” alisema na kuongeza kuwa, mazingira ya uzalishaji kiwandani hapo hayaridhishi ambapo chumvi inayozalishwa inamwagwa kwenye sakafu chafu.

Alisema chumvi iliyofikia kwenye hatua ya kusambazwa kwa walaji inatakiwa kuhifadhiwa sehemu nzuri tofauti na kiwanda hicho kinavyofanya ambapo madhara yanayoweza kusababishwa na matumizi ya chumvi isiyo na madini joto ni pamoja na watumiaji kupata ugonjwa wa kuvimba tezi shingoni (goita).

Naye Mkuu wa Kitengo cha Mahusiano wa TBS, Roida Andusamile, aliwataka wazalishaji kutengeneza bidhaa zao katika viwango vya ubora na kufuata utaratibu waliopangiwa na shirika hilo.

Meneja Msaidizi wa kiwanda hicho, Daudi Chaula, alisema kuwa TBS ilikuwa inachukua sampuri na kwenda kupima lakini hawakuwahi kupata majibu na vipimo vyao vinaonesha madini joto yapo.

“Tukipima na kipimo chetu madini joto yanaonekana lakini TBS wanataka watuelekeze viwango vinavyohitajika,” alisema.

Chanzo:Majira

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Pwani Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa