Home » » RC: TAKWIMU ZA SENSA ZITUMIKE KUPANGA MIPANGO YA MAENDELEO

RC: TAKWIMU ZA SENSA ZITUMIKE KUPANGA MIPANGO YA MAENDELEO

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani,Mwatumu Mahiza.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mwatumu Mahiza amewataka wananchi pamoja na watumishi wa mikoa, wilaya na Halmashauri nchini kutumia takwimu za sensa ya watu na makazi ya  mwaka 2012 kupanga mipango ya kuziletea maendeleo.

Mahiza aliyasema hayo katika semina ya usambazaji wa matokeo ya sensa ya watu na makazi katika mkoa huo  ambayo ilizinduliwa ramsi jana katika ofisi za mkoa wa mkoa wa Pwani mjini Kibaha.

Alisema endapo takwimu hizo zitatumika ipasavyo na kwa usahihi zitasaidia kwa kiwango kikubwa kuleta maendeleo kwa wananchi na nchi nzima kwa ujumla.

“Serikali iliandaa sensa hii kwa lengo la kupata takwimubora zitakazotumika katika kupanga, kutunga sera, kutathmini utekelezaji wa mipango ya maendeleo na utoaji huduma kwa wananchi ili kuchangia kiwango cha maisha cha kila mwananchi,” alisema na kuongeza:

“Kwa kutumia takwimu hizi  ni lazima itawasaidia  kupanga mipango yenu vizuri kulingana na idadi ya watu mlionao katika familia, kijiji, halmashauri au katika mikoa yenu, siyo rahisi wewe una familia kubwa halafu ukapika ugali kidogo ni lazima utapika kulingana na ukubwa wa familia, vivyo hivyo katika halmashauri au mikoa mipango mtakayopanga ni lazima mhakikishe inaendana na idadi ya watu mlionao.”

Aidha, aliitaka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kuanzisha chombo maalum kitakachotumika kudhibiti matumizi na utoaji ovyo wa takwimu zisizo sahihi ambazo zimekuwa zikitolewa na watu mbalimbali na taasisi mbalimbali.

“Ipo haja ya NBS kuanzisha chombo cha Information data control ambacho kitadhibiti matumizi holela ya takwimu, tofauti na ilivyo sasa mtu akiamua kutoa takwimu anatoa hata bila ya kudhibitishwa na chombo husika, hiyo itasaidia, sisi tunafahamu kuwa TBS wa  takwimu ni NBS, hivyo tunahitaji kila takwimu zinazotolewa ziwe zimethibitishwa na chombo hicho,” alisema Mahiza.

Mkurugenzi Mkuu wa NBS, Dk. Albina Chuwa, alisema usambazaji wa matokeo ya sensa hiyo unatarajiwa kuanza kusambazwa hivi karibuni katika mikoa yote nchini, katika wilaya, mikoa na hata vijiji.

Naye Mwakilishi wa Shirika la Idadi ya watu na Makazi Duniani (UNFPA), DK. Collins Opiyo, aliwataka vijana kutumia takwimu hizo katika kutimiza ndoto zao.
 
SOURCE: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Pwani Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa