Home » » WAGONJWA WA AKILI WALALA WODI MOJA NA WENGINE

WAGONJWA WA AKILI WALALA WODI MOJA NA WENGINE

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.


Hospitali kongwe ya Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani, inakabiliwa na upungufu wa wodi za kulaza wagonjwa na kulazimika kuwachanganya wagonjwa wenye matatizo ya akili na wale wenye  maradhi mengine.

Muuguzi wa hospitali hiyo, Bahati Kuguru, alisema hospitali hiyo ni miongoni mwa zile zinazofanya kazi katika mazingira magumu hasa ya kutokuwa na wodi maalum za kulaza wagonjwa hali inayohatarisha usalama wa wagonjwa na wauguzi.

 “Serikali iangalie namna ya kunusuru hali hii haraka iwezekanavyo kwa sababu wagonjwa wenye matatizo ya akili kitabibu wanahitaji kulazwa wodi maalum peke yao, vinginevyo wanaweza kuleta madhara kwa wagonjwa wengine na wauguzi pia,” alisema Kuguru.

Pia alisema chumba cha kuhifadhia wagonjwa  cha hospitali hiyo ni kidogo na hakina majokofu jambo linalosababisha ndugu kulazimishwa kuchukua miili ya ndugu zao muda mfupi baada ya kufariki dunia.

Aliongeza kuwa ingawa serikali inazitambua changamoto zilizoko, bado haijashirikiana na hospitali hiyo katika kuboresha mazingira halisi badala yake miundombinu yake inazidi kuchakaa.

“Tunaomba serikali ichukue maamuzi magumu katika kutatua suala hili, kwanza itupatie gari ya usafiri itakayotumika kutoa huduma ndani na nje ya hospitali pale inapobidi pamoja na kujenga majengo yatakayojitegemea kutokana na tatizo la wagonjwa,” alisema Kaguru.

Mgonjwa wa matatizo ya akili aliyelazwa katika wodi ya wananwake katika hospitali hiyo, Roida Mwangaya, alisema serikali iboreshe hospitali hiyo kwa sababu ni kitovu cha wakazi wa ndani na nje ya eneo hilo.

“Ipatikane wodi  maalumu za kulaza wanawake, watoto, wanaume pamoja na kitengo maalum cha kuwalaza na kuwalea wagonjwa wa matatizo ya akili,” alisema Mwangaya.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Pwani Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa