Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
MKUU wa Mkoa wa Pwani, Mwantumu Mahiza amepiga marufuku wananchi kuchangia mafuta kwa ajili ya magari ya wagonjwa pale wanapopewa rufaa kutoka vituo vya afya kwenye Hospitali ya Wilaya au Tumbi.
Alitoa agizo hilo katika Kijiji cha Miono baada ya kila mwananchi aliyepata nafasi ya kuuliza swali kwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana kulalamikia kutakiwa kutoa fedha kwa ajili ya gari la wagonjwa na kumuona daktari.
Wananchi hao walisema Kituo cha Afya cha Miono kimekuwa kikiwatoza Sh 5,000 kwa ajili ya kumuona daktari na pia kulazimika kutoa Sh 80,000 ya kuchangia mafuta pale mgonjwa anapokuwa amepewa rufaa.
Walisema jambo hilo limekuwa tofauti kwa wangonjwa ambao wamekuwa wakitoka Hospitali ya Wilaya kuhamishiwa Hospitali ya Tumbi wamekuwa hawatozwi kitu na wanalipa Sh 1,000 tu kama gharama za kumuona daktari.
Pia walisema pamoja na kutoa kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya matibabu, lakini wamekuwa hawapati dawa katika vituo hivyo.
Mahiza alisema: “Halmashauri ya Bagamoyo ina shida, nilishawahi kulikataza hili baada ya kulalamikiwa na wananchi, sasa natoa agizo, hakuna mwananchi kuchangia gharama za gari la wagonjwa, na kama itatokea hivyo mnajua namba yangu ya simu nipigieni.”
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri, Shukuru Mbato alisema awali vituo vya afya vilikuwa vikipata mgawo wa lita 350 za mafuta kwa mwezi, ambazo zilikuwa hazikidhi mahitaji, jambo lililofanya kuongezwa hadi kufika lita 500.
“Kwa sababu mafuta yalikuwa hayatoshelezi, tuliamua kuwa wananchi wachangie nusu ya gharama.
Kuhusu fedha zinazotozwa unapokwenda kumuona daktari, Mbato alisema kiwango hicho kiliwekwa ili kuwafanya wananchi waweze kujiandikisha kwenye Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF).
Mbato alisema kutokana na malalamiko ya wananchi, kuanzia sasa wananchi watachangia kiasi cha kawaida cha Sh 1,000 na kuwa hiyo inatokana na hatua ya Halmashauri kujenga jengo la upasuaji litakalopunguza adha ya wananchi wengi kupelekwa hospitali za wilaya na Tumbi.
Chanzo;Habari Leo
0 comments:
Post a Comment