Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
ASASI isiyo ya kiserikali ya Youth Partnership Countrywide (YPC), ya
Kibaha mkoani Pwani, imezindua mpango wa Sauti ya Vijana kwenye
Uwajibikaji (ViVA), utakaowajengea uwezo vijana katika suala la
uwajibikaji kuanzia ngazi ya vitongoji pamoja na kuwashawishi wananchi
kushiriki mipango ya maendeleo.
Mpango huo wa miaka mitatu ambao umezinduliwa juzi mjini hapa na
Ofisa Tarafa wa Kibaha, Anatory Mhango, utazingatia kujenga uwezo kwa
vijana na jamii kwenye maeneo ya uwajibikaji, elimu ya ujasiriamali,
biashara, elimu ya uongozi, elimu ya uraia pamoja na ushawishi na
utetezi wa sera.
Akitoa taarifa ya mpango huo, Mratibu wa ViVA, Samwel Stanley,
alisema pamoja na kulenga kuwajengea uwezo vijana, pia wanawajengea
uwezo wananchi katika kushawishi kushiriki kwenye michakato ya maendeleo
na kuchochea ufanisi na utendaji wa serikali za mitaa katika Wilaya za
Kibaha na Mafia.
Stanley, pia alisema kuwa mradi huo utaendeshwa vijiji 24 vya Wilaya
ya Kibaha na 12 Mafia, ambavyo wananchi wake watapatiwa elimu ya masuala
ya kodi ili kuweza kufuatilia ulipwaji wa kodi kutoka kwenye kampuni
kubwa zilizowekeza kwenye halmashauri zao.
“Mpango huu ambao utagharimu sh milioni 450 hadi kukamilika, tumepata
ufadhili kutoka shirika la Action Aid, tumebaini changamoto nyingi
kwenye kusukuma gurudumu la maendeleo, hivyo katika kuhakikisha
tunashirikiana na serikali kufanikisha hili, mpango huu umekuja kutoa
elimu kwa vijana na wananchi katika Wilaya za mradi,” alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa YPC, Israel Ilunde, alisema kupitia
mafunzo mbalimbali yatakayokuwa yakitolewa kwenye mradi huo wa vijana,
watapata uelewa wa kujipanga na kuleta ushawishi kwenye mipango na
bajeti ili kuwa na huduma bora zaidi za kijamii katika wilaya zao.
0 comments:
Post a Comment