Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
MWENYEKITI wa Kijiji cha Mlamleni Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani,
Hamisi Linyimuka (CCM), amewaomba radhi wazee wa mtaa wa Videte kwa kosa
la kumilikisha ardhi.
Hatua hiyo ilikuja baada ya Mwenyekiti huyo, kugawa eneo la Ofisi ya
mtaa kwa mkazi wa Dar es Salaam, Shamila Masawe, kinyume cha sheria.
Mwenyekiti huyo, aliwekwa kitimoto na wazee wa mtaa huo katika kikao
kilichoitishwa juzi na Ofisa Mtendaji wa Kata ya Tambani, Abasi Likonda,
ambacho kilikuwa kikijadili kwa kina juu ya tuhuma hizo.
Akizungumza kwa niaba ya wazee hao, Omary Silima alisema katika eneo
hilo ambalo tayari ujenzi wa ofisi unaendelea, walitenga eneo lenye
upana wa mita 18 na urefu mita 40 ambalo wanatarajia kuchimba kisima kwa
ajili ya huduma ya maji kwa kazi wa mtaa huo.
“Eneo alilomilikishwa huyu Masawe ni la kwetu tumenunua kwa nguvu
zetu wenyewe, lakini mwenyekiti ameliuza bila ya kutushirikisha jambo
ambalo tunapingana nalo kwani anatumia uongozi wake vibaya,” alisema.
Naye mwenyekiti wa mtaa huo, Yusufu Kigundula maarufu kama Lule,
alisema alishangazwa na mwenyekiti huyo kumtaka aandike hati ya pili ya
eneo hilo, na kwamba eneo hilo litakapochimbwa kisima, Masawe atachota
maji mpaka mwisho wa maisha yake bila kulipia.
Hata hivyo, Lule alisema eneo hilo litabaki kuwa la serikali na
kisima kitakachochimbwa kitakua cha serikali na kitatumiwa na wananchi.
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment