Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
MKUU wa Mkoa wa Pwani, Mwantumu Mahiza, amewataka wakazi wa Mkoa wa
Pwani kujitokeza kwa wingi kwenye usajili na utambuzi wa watu kwa
ajili ya vitambulisho vya taifa.
Zoezi hilo ambalo linatarajiwa kuanza leo katika maeneo ya mkoa huo,
linatarajiwa kufanywa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA),
ambapo viongozi kuanzia ngazi ya wilaya wametakiwa kutoa ushirikiano,
ili kufanikisha zoezi hilo.
Mahiza alisema atahakikisha analisimamia vizuri zoezi hilo, ili
liweze kufanikiwa, hivyo kuwaomba wakuu wa wilaya na wakurugenzi
kuhakikisha zoezi hilo linafanikiwa kama serikali ilivyoagiza.
“Tunapaswa kuwapa NIDA ushirikiano, ninawaagiza viongozi wote wa mkoa
huu muwapatie maelekezo watendaji waliopo chini yenu, pia mshiriki
kutoa elimu kwa umma, kusimamia na kuendesha zoezi la usajili na
utambuzi katika maeneo yenu ya utawala,” alisema Mahiza.
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa, Dickson Maimu,
alisema zoezi hilo linaingia Mkoa wa Pwani baada ya usajili Zanzibar
na Mkoa wa Dar es Salaam.
Maimu alisema mbali ya usaili, muda mwingi utatumiwa na watendaji
kuhakiki taarifa za waombaji wa vitambulisho vya taifa, ili kuwa na
taarifa sahihi za watu.
Mkurugenzi huyo aliishukuru serikali kwa kuwapatia fedha za kuendesha
zoezi hilo, na kwamba watakapomaliza Mkoa wa Pwani watahamia katika
mikoa ya Lindi, Mtwara, Morogoro, Tanga na Kilimanjaro
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment