Home » » MAMA SHUJAA WA CHAKULA WAWAHIMIZA WATOTO WAO KUJIHUSISHA ZAIDI NA KILIMO.

MAMA SHUJAA WA CHAKULA WAWAHIMIZA WATOTO WAO KUJIHUSISHA ZAIDI NA KILIMO.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 




Siku hii ni yenye balaa kwa wanakijiji cha Maisha Plus kutokana na matukio yaliyotokea ambayo matokeo yake si mazuri kwa wanakijiji hao. Awali ya yote asubuhi kama kawaida walifanya usafi wa mazingira na kaya zao huku wanakijiji wengine wakiongea na babu kuhusiana na kilichojiri kijijini hapo. Kulikuwa na uvumi ya kwamba kuna mwanakijiji mmoja asiyetambulika anawachawia wenzake usiku wanapolala pasipokujua ni nani anayefanya hivyo. 

Baadhi ya wanakijiji hao walikuwa wakimshuku kijana Boniphace Meng’anyi kuwa inawezekana ikawa ni yeye ingawa hawakuwa na ushahidi wowote bali wanahisi tu. Hii inatokana na kwamba kijana huyo hana uwoga na huwa na desturi ya kwenda kisimani usiku kuoga na kufanya shughuli zake nyingine. 

Tabia ya kijana huyu iliwafanya baadhi ya wanakijiji kuwa na wasiwasi naye zaidi kuhusika na kitendo hicho ingawa mpaka sasa hawana uhakika wa mtu anayehusika kuchawia wenzake usiku walalapo. 


Pamoja na matukio mengine kutokea hapo kijijini haikuwazuia wanakijiji kubadilishana mawazo na kujadili masuala mbalimbali yanayowahusu. Mambo mbalimbali yalijadiliwa ikiwa ni pamoja na malengo waliyokuwa nayo wanakijijii baada ya kutoka hapa katika kijiji cha Maisha Plus. 

Wengi wao waliahidi kuendeleza walichokipata kwa kuelimisha jamii inayowazuka, kujiajiri kwa vijana na kupanua miradi waliyokuwa nayo ili waweze kupiga hatua katika kujiletea maendeleo. 

Mama Shujaa wa Chakula walichukua fursa hii kuwasisitiza watoto wao kujishughulisha na kilimo kwani kinaleta tija kwa mkulima na taifa kwa ujumla badala ya kuzurura mitaani na kukaa vijiweni.


Kizaa zaa kilitokea kijijini baada ya yai walilokabidhiwa wiki kadhaa zilizopita kuvunjika. Yai hilo lina historia ndefu ambapo hapo awali yai lilifichwa na atakaye bahatika kulifichua litamlinda kwa maana hatatoka kwenye mashindano hata kama atakuwa kwenye orodha ya mchujo. 

Farida Ally kutoka Pwani alifanikiwa kupata yai la kwanza lakini kwa bahati mbaya lilivunjika baada ya kukaa nalo kwa siku chache hivyo kuingia moja kwa moja katika orodha ya mchujo. 

Kwa kuwa walitakiwa washiriki watano kuaga mashindano hayo kipindi hicho naye alikuwa miongoni mwa waliotolewa iliyofanya washiriki wengine kuwa makini katika kufanya maamuzi wa jambo kama hili. 

Baada ya yai hilo kuvunjika siku ya pili yake lililetwa yai jingine ambapo nafasi ilitangazwa kwa aliyetayari kulitunza na lenyewe kumlinda asiweze kutoka katika kinyang’anyiro cha Maisha Plus 2014. 

Tukio lile liliwafanya washiriki wengine kusita kuchukua jukumu hilo litakaloweza kuwatia matatani pasipokupenda hivyo walikataa kulipokea na ndipo hapo lilihifadhiwa uwanjani katika kijiji hicho. 

Wanakijiji walifanya jitihada zote kulinda yai hilo lisije kuvunjika na wakati mwingine wanakijiji hao hawalali usiku kuhakikisha lipo salama. 

Jitihada za wanakijiji ziligonga mwamba pale yai lilipovunjika kutokana na joto lililopo kwani lilikuwa katika sehemu ya uwazi ambapo hukabiliwa na mvua, jua na baridi. 

Yai hili lilisadikika kuvunjika siku mbili au tatu zilizopita ila wanakijiji walipata hofu kubwa baada ya kusikia taarifa hizo kwani walijua kabisa tayari wapo matatani na wameshazua balaa kijijini hapo hivyo kusita kutoa taarifa kwa wahusika na kukaa kimya. 

Balaa watakalopata ni kukaa na njaa na kupewa adhabu ambayo hawaijui itakuwa ni ya aina gani hivyo kuzidisha hofu zaidi miongoni mwa wanakijiji. Babu na Masoud Kipanya wameshasikia habari za kuvunjika kwa yai kijijini na haieleweki ni hatua gani watakayoichukua 

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Pwani Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa