Home » » MVUA YAMEZA DARAJA L RUVU

MVUA YAMEZA DARAJA L RUVU

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Mkuu wa mkoa wa Pwani Mwantumu Mahiza akiwa katika eneo la daraja la mto Ruvu kushuhudia hali ilivyo.(Picha:Selemani Mpochi)
Maelfu  ya abiria wamekwama baada ya magari waliyokuwa wakisafiria kwenda baadhi ya mikoa nchini kukwama katika maeneo ya Ruvu Sekondari, Ruvu Darajani mkoani Pwani na Kongowe jijini Dar es Salaam.
Waandishi wa NIPASHE walishuhudia mamia ya magari hayo yakikwama baada ya kushindwa kushindwa kupita katika barabara kuu ya Dar es Salaam-Morogoro, eneo la Ruvu Sekondari, wilayani Kibaha na Ruvu Darajani, wilayani Bagamoyo, Mkoani Pwani, baada ya mto Ruvu kufurika na maji kuziba njia na madaraja, kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha katika mikoa ya Ukanda wa Pwani.

Abiria hao waliokwama katika barabara hiyo kwa zaidi ya saa 15 Aprili 13, mwaka huu ni wale waliokuwa wakisafiri kuelekea mikoa ya Morogoro na Tanga .

Na wengine ni wale waliokuwa wakiafiri kwenda mikoa ya Kusini (Lindi na Mtwara) baada ya daraja la mto Mzinga uliopo Kongowe kubomoka na kusombwa na mafuriko.
 
ATHARI YA MVUA KIBAHA, BAGAMOYO
Mbali na kukatika kwa mawasiliano ya usafiri kufuatia mto huo kufurika, pia nyumba zaidi ya 10 zilizojengwa kwa saruji zimebomoka, huku nyigine zaidi ya 20 zilizojengwa kwa udongo zikiripotiwa kumomonyoka kabisa huku nyasi zilizokuwa zimetumika kuezeka zikisombwa na mafuriko.

 Ramadhani Mnyamani na Said Mtotole, ambao ni wakazi wa maeneo hayo, kwa nyakati tofauti walisema maji yaliyosambaa eneo lote hilo hayajasimama, bali yanatembea kwa kasi kutokana na mto Ruvu kufurika baada ya mvua kunyesha kwa siku tatu mfululizo.

Walisema hali hiyo imesababisha mafuriko, hususan katika eneo la darajani.

KAULI YA KAMANDA WA POLISI
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Ulrich Matei, amethitibisha kukwama kwa magari hayo pamoja na abiria.

Aliwataka wananchi wenye lengo la kusafiri kuelekea mikoani kupitia eneo hilo, kuangalia uwezekano wa kuahirissha kama hakuna ulazima kuliko kuendelea  wakati njia ipo mashakani kutokana na mvua zinazonyesha.

“Naomba kama mtu hana ulazima wa kusafiri kwa sasa kuelekea mikoani, abaki kwanza, aangalie usalama wake. Na kama safari hiyo ina ulazima, basi watafute njia mbadala ya kupitia kutokea Dar es Salaam. Mfano, wapitie Bagamoyo wakatokee Msata na kuendelea na safari, kama Tanga sawa. Na kama Mororgoro, arudi hadi Chalinze kisha aende zake,” alisema  Matei.

Alisema kwenye matatizo siyo lazima mtu aambiwe, ila kutokana na hali halisi, hapana budi kutoa ushauri ili kuepusha matatizo kwa abiria au mtu anayetaka kutumia barabara hiyo kuwa kwa sasa haipitiki kutokana na uharibifu wa miundombinu na baadhi ya magari kukwama.
 
JK ATEMBELEA DARAJA MTO RUVU
Rais Jakaya Kikwete alifika katika eneo hilo na kuzungumza na wananchi na kuwataka wawe wavumilivu kwa kuwa ni janga la kitaifa.

 Rais Kikwete alisema kama kiongozi wa serikali   hali hiyo inamuumiza japo haiwezi kuzuilika.

“Kwa kweli tuwe wavumilivu. Nimeagiza jeshi wahakikishe usalama na maji yatakapopungua mtaruhusiwa kupita na kuendelea na safari japo tunajua mmechelewa,” alisema Kikwete.

Alisema ni muhimu wananchi wakawa wanapenda kufuatilia vyombo vya habari ili kujua hali ya nchi inavyokwenda, kwani toka jana ilionekana wazi kuwa kuna maeneo hayatapitika ikiwamo Pwani.

Katika tukio hilo lililochangia kifo cha mtoto wa mwaka mmoja na nusu baada ya kuugua ghafla kutokana na  hali ya hewa kubadilika.

MAHIZA ANENA
Akizungumzia tukio hilo, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mwantumu Mahiza, aliwataka wasafiri wote pamoja na wananchi kuwa watulivu mpaka hali itakapotulia na kuruhusu gari kuanza kupita.

“Tunawaomba jamani watu kuwa watulivu. Nimeagiza wanaofanya biashara ya chakula kutopandisha bei, huku Jeshi la Wananchi likiagizwa kupunguza bei ya chakula katika baa yao, iliyopo eneo hilo,” alisema Mahiza.

Aliiomba Mamlaka ya Usafirishaji Majini na Nchi kavu (Sumatra) kuzuia magari kusafiri mpaka kutakapokuwa na uhakika wa hali ya hewa na kuwataka wafanyabiashara kuwa na utu na kuacha kupenda fedha kunapokuwa na majanga kama hayo.

Wakizungumzia hali hiyo, baadhi ya abiria walisema imewaletea karaha katika safari yao  kwani walitegemea kufika mapema lakini hawajui kama kuna uwezekano wa kupita.

Shabani Issa,  abiria wa basi la Musoma Express linalofanya safari zake Dar-Musoma alisema: “Namuachia Mungu kwa kweli. Maana sijui hatma yangu nini mpaka sasa, ikitokea nakwenda sawa ikitokea nimekwama sawa. Nimechanganyikiwa kabisa.”

Juma Kaiko, ambaye ni abiria wa basi la Kampuni ya Saibaba ya Arusha, alisema: “Mimi naenda msibani nimefiwa na mama yangu mzazi wanazika saa 10 jioni na mfukoni nina hela ya nauli tu. Kwa hiyo, nimepata pigo kubwa sana.” 

 NDUGAI AKWAMA
Adha hiyo pia iliwakuta baadhi ya viongozi  akiwamo Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai na kulazimika kuungana na wananchi kusubiri saa kadhaa katika eneo hilo.

Ndugai aliwataka baadhi ya madereva kuwa wasikivu kutii amri ya Serikali inapotolewa ili kuepuka maafa.

“Hii hali hakuna wa kumlaumu, maana viongozi wanatoa taarifa, lakini  matokeo kama haya ni Mungu anapanga na kutekeleza mwenyewe,” alisema Ndugai.
Hata hivyo, hali ilianza kutengemaa na magari kuruhusiwa kupita kuanzia saa 11 jioni.

DARAJA MSUGUSUGU LAVUNJIKA
Wakati huo huo; katika barabara hiyo eneo la Msugusugu daraja limevunjika na kusababisha magari mizigo kushindwa kuendelea na safari.

MTO MZINGA WAKWAMISHA ABIRIA

Wakati hali ikiwa hivyo katika daraja la mto Ruvu, maelfu ya abiria waliotarajia kusafiri kwenda mikoa ya Kusini (Lindi na Mtwara) jana walishindwa kufanya hivyo baada ya daraja la Mto Mzinga lililopo eneo la Kongowe, jijini Dar es Salaam, kubomoka na kusombwa na mafuriko  kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha jijini humo na mikoa ya jirani.

Akizungumza na NIPASHE jana, mmoja wa mashuhuda, Hamisi Mohamed, ambaye ni mkazi wa Kongowe, alisema daraja hilo lilibomoka jana, majira ya saa 12:00 asubuhi baada ya mabasi matatu kuvuka.

Alisema mbali na daraja hilo kubomoka, pia nyumba tisa zilizokuwa na familia zaidi ya 15 zilisombwa na mafuriko na nyingine kujaa maji, ikiwamo  yake.

Kwa mujibu wa shuhuda huyo, hali hiyo imesababisha zaidi ya familia 50 kukosa makazi kutokana na kusombwa na mafuriko.

“Daraja lilibomoka saa 12:00 asubuhi leo (jana) na kufanya msururu wa mabasi yaendayo mikoa ya Kusini kushindwa kufanya safari zake... pia familia zaidi ya 50 hazina makazi baada ya nyumba tisa kubomoka na nyingine zaidi ya 110 kujaa maji,” alisema Mohamed.

 “Mimi mwenyewe nimeihamisha familia yangu baada ya nyumba yangu kujaa maji, ”  aliongeza.

Alisema kutokana na daraja hilo kubomoka, watu walioko upande wa Kongowe na Mbagala hawezi kuvuka kutoka upande mmoja kwenda mwingine.

NIPASHE ilishuhudia msururu wa mabasi ya abiria yanayofanya safari zake kwenda mikoa hiyo, huku yakiwa na abiria.

Mwanafunzi wa Chuo cha Uuguzi Kimara jijini Dar es Salaam, Fridah Mwidadi, alisema alitarajia  kusafiri na kufika Wilaya ya Newala mkoani Mtwara jana kufanya mazoezi ya vitendo katika Hospitali ya Wilaya hiyo, lakini safari yake iliishia Mbagala baada ya uongozi wa basi la Ibra kuomba radhi saa 6:30 mchana kwa kuahirisha safari hiyo.

KAWE WABOMOA NYUMBA ZAO
Pia baadhi ya wakazi wa Kawe wanaoishi pembezoni mwa mto Mbezi jijini Dar es Salaam, jana walilazimika kubomoa nyumba zao kutokana kwakuhofia  kuharibika.

NIPASHE lilishuhudia wakazi hao wakihaha kubomoa nyumba zao, kung’oa madirisha, milango na mabati ili kunusuru zizisombwe na mafuriko  huku nyingine zikijaa maji na kuzolewa.

 Wakizungumza na NIPASHE baadhi yao, walisema wameamua kubomoa nyumba hizo ili kuokoa mabati, madirisha na milango kuliko kuacha vikisombwa na mafuriko.

 Mmoja wa wamiliki wa nyumba kwenye eneo hilo , Ally Abdalah, alisema hakutegemea kama mto huo unaweza kufurika na kuleta madhara makubwa na kwamba, alilazimika kuwaamuru wapangaji wake kuhamisha mali zao kabla ya maji kujaa ndani ya nyumba.

Hawa Hamisi alisema amelazimika kuhamisha vitu vyake na kuvipeleka mbali ili kuepusha uharibifu na kunusuru maisha yao na watoto wao kutokana na nyumba hizo kuanza kujaa maji.

“Hapa nilipo sina fedha ya kupanga nyumba nyingine na kwenye nyumba hii mkataba wangu haujaisha. Kwa sasa nimehifadhi vitu kwa ndugu zangu…hatima yangu siijui na nyumba ndiyo hiyo imebomoka,” alisema.

Waliiomba serikali kuwasaidia kila yanapotokea majanga kwa watu wa maeneo ya Jangwani, Kigogo na Mbuyuni.

Imeandikwa na Kamili Mmbando, Hellen Mwango, Enles Mbegalo (Dar) na Julieta Samsoni (Pwani).
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Pwani Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa