Home » » CCM YACHANJA MBUGA CHALINZE

CCM YACHANJA MBUGA CHALINZE

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
  Vijana wasusia uchaguzi
Mmoja wa wapiga kura katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Chalinze aliyejitambulisha kwa jina moja la Sabina, akitumbukiza karatasi ya kura kumchagua mbunge wake jana.PICHA:MPIGAPICHA WETU
Uchaguzi  mdogo katika Jimbo la Chalinze mkoani Pwani, jana ulifanyika kwa utulivu huku matokeo ya awali yakionyesha mgombea kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ridhiwani Kikwete, akiwaburuza kwa mbali wagombea wenzake kutoka vyama vya upinzani.
Matokeo ya awali yaliyopatikana katika baadhi ya vituo vya jimbo hilo yalionyesha kama ifuatavyo:-

Kituo cha Afya Chalinze CCM kura 44, Chadema (14), CUF (3), AFP (0) na NRA(0); Ofisi ya Mtendaji namba 3 CCM (43), Chadema (17), CUF (2), NRA (0) na AFP (0) na Ofisi ya Mtendaji namba 2 CCM (40), Chadema (17), CUF (7), AFP (0) na NRA (0).

Kituo cha Msata CCM (74), Chadema (5), CUF (1), AFP (0) na NRA (0); Kituo cha Mdaula CCM (36), Chadema (5), CUF (0), AFP (0) na NRA (1); Shule ya Msingi Chaua CCM (80), Chadema (2), CUF (2), AFP (0) na NRA (0).

Kituo cha Sangasanga (CCM 34), Chadema (2), CUF (0), NRA (0) na NRA (0); Kituo cha Mikoroshini namba 1 CCM (30), Chadema (11), CUF (3), NRA (0) na AFP (0); Kituo cha Mikoroshini namba 2 CCM (32), Chadema (11), CUF (7), NRA (0) na AFP (0).

Kituo cha NMC namba 1 CCM (34), Chadema (12), CUF (5), AFP (0) na NRA (1); Kituo cha NMC namba 3 CCM (33), Chadema (14), CUF (4), AFP (0) na NRA (0); Kituo cha Shule Msingi Bulengu namba 1 CCM (67), Chadema (14), CUF (4), NRA (0) na AFP (0); Kituo cha Shule ya Msingi Bulengu namba 2 CCM (58), Chadema (10), CUF (10), NRA (0) na AFP (0).

Aidha, matokeo hayo ya awali, yanaonyesha pia kuwa karibu vituo vyote vya Kata ya Mbwewe, hadi tunakwenda mitamboni, CCM ilikuwa ikiongoza.

Aidha, uchaguzi huo ulishuhudia wapigakura wachache wakijitokeza wengi wakiwa ni wazee.

Hali hiyo, ambayo ilishuhudiwa na NIPASHE iliyozungukia vituo mbalimbali vya kupigia kura, inadaiwa kuwa inatokana na vijana kugoma kujitokeza kupiga kura kwa madai kuwa hata watakayempigia kura, hawezi kuwaletea maendeleo katika jimbo hilo.

Baadhi ya vijana waliozungumza na NIPASHE walisema huu ni msimu wao wa kupalilia mahindi, hivyo wanaenda kulima, kwani ndilo jambo pekee litakalowasaidia kuliko kupiga kura ambayo inawapa kula watu wengine.

Hata hivyo, walisema wamekuwa wakihudhuria mikutano ya kampeni kutokana na kuhamasishwa na baadhi ya vyama vya siasa ili waijaze, lakini wakasema hawakuwa wakiitilia maanani.

NIPASHE ilishuhudia kata ya Mbweni ikiwa ina wapigakura 461 waliojiandikisha kupiga kura, lakini waliojitokeza kupiga kura jana walikuwa ni 30 tu huku idadi kubwa ikiwa ni wazee.

Katika Kata ya Kibindu kituo cha Kikomba, waliojiandikisha kupiga kura ni 450, lakini waliojitokeza kupigakura walikuwa ni 50.

Kwa mlolongo huo huo, katika kituo cha Kibindu Shuleni waliojiandikisha kupiga kura ni 378, lakini waliojitokeza kipiga kura ni 100, wakati Kwa Msanga waliojiandikisha ni 277 waliojitokeza kupiga kura ni 60.

Hali hiyo ilijitokeza katika vituo vingi katika kata za Bwilingu, Ubena, Zomozi na Msata tofauti na idadi iliyoko kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura kwa sababu ambazo hazijajulikana.

Baadhi ya wasimamizi wa uchaguzi katika maeneo hayo walionekana wakiwa hawana kazi baadhi yao ‘wakichati’ na simu zao za mikononi.

KIKWETE: NIMEMPIGIA KURA MGOMBEA WA CCM

Wakati hali ikiwa hivyo, Rais Jakaya Kikwete na mkewe, Mama Salma, walipiga kura kijijini kwao, Msoga katika Kituo cha Shule ya Msingi Msoga.

Rais Kikwete aliwasili katika kituo hicho saa 3:22 asubuhi na kupiga kura saa 3:25 asubuhi, baada ya kutanguliwa na mkewe, Mama Salma.

Akizungumza na waandishi wa habari waliokuwa kituoni hapo, Rais Kikwete alisema anafurahia kutimiza haki yake ya kikatiba ya kupiga kura na kwamba amemchagua mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

“Nimefurahi, kwa sababu nimepiga kura na nimemchagua mgombea wa CCM,” alisema Rais Kikwete.

Akizungumzia hali ya upigaji kura na mchakato ulivyo, alisema hajui chochote kwani alifika katika kijiji hicho juzi, hivyo hajui taratibu za zoezi hilo.

HALI KATIKA VITUO

NIPASHE lilipita katika vituo kadhaa kuanzia saa 1:00 asubuhi hadi saa 5:00 asubuhi na kushuhudia hali ikiwa shwari, huku waliojitokeza kupiga kura wakiwa wachache.

Katika kituo cha Shule ya Msingi Msoga, watu waliowahi walikuwa wachache na walipohojiwa kuhusu hali hiyo, walisema ni kutokana na wengi kuanzia mashambani.

“Watu watakuja tu. Bado muda. Wengi watakuwa wameanzia shambani na wengine wanawaandalia watoto uji asubuhi. Kwa hiyo watakuja tu muda bado,” alisema mmoja wa wapigakura.

Hali ilikuwa hivyo kwa vituo vya kata ya Pera na Msoga pia.

Msimamizi Mkuu wa Kituo cha Shule ya Msingi Msoga, Christina Mkenda, alisema hali ni nzuri na changamoto iliyopo ni watu watano waliorudishwa kutokana na kukosa vigezo.

Alisema watu watatu walikuwa na kadi za kupiga kura, lakini majina yao yalikuwapo na hawakuwa na vithibitisho vya kutakiwa kufanya hivyo na kwamba wawili walikosa majina yao katika kituo hicho.

MGOMBEA WA AFP
Mgombea ubunge kupitia Chama Cha AFP, Ramadhani Mgaya, alipiga kura katika Kituo cha Afya, kata ya Bwilingu, saa 4:00 asubuhi akiwa peke yake.

Alisema hali ya uchaguzi ni nzuri japokuwa kuna kasoro ndogo ndogo zinazofanywa na mawakala na kwamba atazitolea taarifa kwa Jeshi la Polisi.

“Kasoro zipo. Tunaona viongozi wa CCM wanaleta watu na magari, halafu kuna mtu mwingine kwenye kituo anawasalimia kwa mikono. Kwa hiyo, nahisi atakuwa anawapatia kitu,” alisema Mgaya.

Akizungumzia namna alivyojipanga kupokea matokeo, alisema yuko tayari kwa matokeo na amejiandaa kwa kushinda na kama akishinda atajipanga kukabiliana na changamoto za jimbo hilo.

“Kila mgombea atavuna alichopanda katika kampeni tulizofanya. Hivyo, jukumu lililobaki ni kwa wananchi kufanya uchaguzi wa kumchagua wanayemtaka,” alisema.

Alisema kama hatashinda utakuwa muda mwafaka wa yeye na chama chake kukaa chini ili kufanya tathmini ya hali ya uchaguzi ili wajipange kwa uchaguzi ujao mwakani.

Akizungumzia hali ya kushambuliwa kwake na kujeruhiwa mkono wake wa kulia siku chache kabla ya uchaguzi, alisema haamini kama waliomshambulia wana ugomvi wa kisiasa na kwamba, ameliachia Jeshi la Polisi kesi hiyo.

 MGOMBEA WA CCM APIGA KURA
Mgombea ubunge wa jimbo hilo (CCM), Ridhiwani Kikwete, aliwasili katika kituo cha kupigia kura cha Ofisi ya Mtendaji, kata namba 3 saa 4:30 asubuhi akiwa na mkewe, Arafa Ridhiwani na watoto wao, Azina na Haiman.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kupiga kura huku akiwa na furaha, Ridhiwani alisema amefurahi kutumia haki yake ya kidemokrasia na kwamba anaamini wengi watamuunga mkono.

“Nina furaha kwa sababu ya kutimiza haki yangu. Na pia naamini nitashinda. Ila kitakachoninyima furaha labda ni uchache wa asilimia. Lakini nimemaliza kazi. Ninachosuburi ni matokeo na mimejiandaa vizuri kuyapokea,” alisema Ridhiwani.

Akizungumzia hali halisi ya upigaji kura, alisema hadi sasa hajasikia kasoro wala malalamiko kwa sababu muda huo alikuwa hajazunguka katika vituo vya kupigia kura.

“Nafikiri baada ya kupiga kura ndiyo nitaanza kuzunguka katika vituo kuangalia hali halisi. Kwa hiyo nadhani nitafahamu baada ya hapo picha kamili,” alisema Ridhiwan.

MGOMBEA WA CHADEMA
Mgombea ubunge kwa tiketi ya Chadema, Mathayo Torongey, alionekana akikagua hali ya usalama na vituo kabla ya kupiga kura.

Akiwa katika Kituo cha Afya, kilichopo kata ya Pera, aliwataka mawakala wa kituo hicho kutokubali kuwapigisha kura watu wasiokuwa na sifa.

Akizungumza na waandishi wa habari alisema hofu yake ni kuwa watu wanaweza kutoka jijini Dar es Salaam kwenda kupiga kura Chalinze kwa kutumia shahada za watu waliokwishafariki dunia.

“Wasiwasi wangu watachukua vitambulisho vya watu wawashawishi mawakala wawaruhusu kupiga kura huku wakiwa hawana vigezo, kwani idadi ya watu wengine waliojiandikisha mwaka 2010 walishafariki dunia,” alisema Torongey.

Akizungumzia hali ya uchaguzi kama atashinda kwa asilimia ngapi au la na namna alivyojiandaa kwa matokeo, alisema yeye ni mtu mdogo sana na kwamba uchaguzi ni mzito.

MKURUGENZI WA UCHAGUZI
Akizungumzia hali ya uchaguzi, Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo hilo, Samweli Sariangi, alisema ni nzuri kwani muda huo alikuwa hajapata kasoro wala malalamiko.

“Ni mapema mno kuzungumzia. Bado watu wengi hawajapiga kura. Hivi nimezunguka takribani vituo 10. Nimeona hali ni nzuri. Siwezi kutoa takwimu sasa hivi. Ila hadi sasa hali ni nzuri na idadi ya waliojiandikisha mwaka 2010 ni 92,939,” alisema Sariangi.

Akizungumzia tatizo la wagombea kubadili vituo vya kupigia kura, alisema ni haki na kwamba mgombea anaweza kuomba kibali cha kubadilishiwa kituo kwa kupewa fomu namba 17.

MGOMBEA ADAI KUWINDWA KWA SILAHA ZA JADI

Katika hatua nyingine, uchaguzi huo uliingia dosari baada ya mgombea ubunge wa jimbo hilo kupitia Chadema, Torongey kudai anawindwa na watu wasiojulikana kwa lengo la kumdhuru.

Akizungumza na waandishi wa habari, Torongey alisema akiwa katika harakati za kuzunguka katika vituo vya kupigia kura, aliona gari aina ya Land Cruiser likimfuatilia  kutoka eneo la Mdaula hadi Ubena.

Alisema alifika Ubena na kuripoti suala hilo kwa polisi waliokuwa katika shughuli za kusimamia uchaguzi na kuwaeleza tukio hilo, ambamo polisi walilisimamisha  na kulipekua na kukuta kuna mapanga, nondo, mikuki na mishale.

Aidha, polisi hao waliamuru gari hilo lenye namba za usajili T 630 BFJ liende kituoni waliokuwa kwenye gari hilo lililokuwa na watu zaidi ya 10 walisema wataenda polisi kwa muda wao wanaenda kwenye kazi zao maeneo ya Bwawani.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Ulrich Matei, akizungumza na waandishi wa habari alithibitisha mgombea huyo kuripoti tukio hilo katika kituo cha polisi na kuagiza kikosi cha polisi kulisaka na kulikamata na baadaye kutoa taarifa zaidi kwa vyombo vya habari.

KADI ZA KUPIGA KURA ZADAIWA KUKUSANYWA
Katika matukio mengine, maeneo ya Ubena baadhi ya wakazi wamelalamikia waandishi wa habari kushindwa kupiga kura kwa madai kuwa kabla ya uchaguzi  kuna baadhi ya makatibu kata wa CCM walipita majumbani kwao kukusanya shahada zao kwa lengo la kuzihakiki lakini hawakurudishiwa.

Katibu Kata wa Tawi la Lulenge, Ubena Rajab Said, alipoulizwa juu ya kuwanyanganya baadhi ya wananchi kadi zao za kupiga kura, alikataa na kusema kuwa ni uzushi mtupu.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Pwani Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa