Home » » CCM YAMTAKA PROF.TIBAIJUKA KWENDA KUTATUA MIGOGORO YA ARDHI

CCM YAMTAKA PROF.TIBAIJUKA KWENDA KUTATUA MIGOGORO YA ARDHI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Profesa Anna Tibaijuka.
Waziri  wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, ametakiwa kumaliza migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji.
Pia ametakiwa kuhakikisha watendaji wake katika wizara hiyo wanatoka ofisini na kwenda kusikiliza matatizo ya wananchi kuhusiana na ardhi badala ya kukaa ofisini na kufunga tai wakati migogoro inaendelea.

Kauli hiyo ilitolewa juzi na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi(CCM), Nape Nnauye wakati akimnadi mgombea wa chama hicho katika Jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete.

Alisema amezunguka maeneo mengi nchini likiwamo Jimbo la Chalinze ambako kila alikopita kumnadi amekutana na kero za migogoro ya ardhi hasa kati ya wakulima na wafugaji.

"Haiwezekani tunasema tuna Waziri lakini hakuna hatua ambazo zinaonekana kuchukuliwa katika kutatua tatizo hilo hasa Chalinze. Mawaziri na watendaji wa serikali acheni kukaa ofisini, nendeni mkasikilize na kutatua kero za ardhi zinazowakabili wananchi," alisisitiza.

Alisema kuendelea kwa migogoro ya ardhi kunatokana na Waziri husika na watendaji wake kutowajibika kuitatua ufumbuzi.

Alisema iwapo Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ingewajibika ipasavyo kero hizo zingepatiwa ufumbuzi.

Nape alimtolea mfano Waziri wa Ujenzi Dk. John Magufuli kuwa ni Waziri ambaye anakwenda katika maeneo yake ya kazi hivyo anajua takwimu na kila kinachoendelea na kutafuta ufumbuzi.

Alisema kitendo hicho cha Dk.Magufuli kufanya kazi kwa kwenda maeneo ya kazi kinapaswa kuigwa na mawaziri  wengine na watendaji wa serikali.

Naye mgombea wa CCM, Ridhiwani, akizungumza katika vijiji vya Mindu Turiani, Makombe na Kizwagi vilivyopo Kata ya Lugoba, alisema endapo atakuwa Mbunge wa Chalinze atahakikisha anakuwa bega kwa bega na viongozi wengine katika kutatua kero zinazowakabili wananchi wa jimbo hilo.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Pwani Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa