Home » » Wafanyabiashara walia na ushuru

Wafanyabiashara walia na ushuru

USHURU wa mabango na kodi nyingine zinazotozwa kwa wafanyabiashara wa mji wa Mailimoja zimeelezwa kuwa ni changamoto kubwa kwa wafanyabiashara.
Akizungumza wakati akikabidhi zawadi mbalimbali kwa wateja walionunua simu kwenye duka la Kampuni ya Lipwai lililopo Mailimoja mjini hapa, Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Mohamed Lutambi, alisema kodi hizo ndizo hasa zinazowakwamisha baadhi yao kuendelea kibiashara.
Lutambi alisema kodi kubwa za leseni za biashara, ushuru wa biashara pamoja na ushuru wa mabango bado ni changamoto kubwa kwao kutokana na kutumia fedha nyingi kulipa kodi kwenye biashara wanazoendesha.
Alisema malengo ya kampuni hiyo ni kufanya biashara kubwa katika mji huo kwa kuwawezesha wakazi wa Mailimoja kupata mahitaji yote wanayofuata nje ya mji huo.
Alieleza wakati wakianzisha biashara hiyo mwaka 2004 walikumbana na changamoto ya soko pamoja na upatikanaji wa mitaji ambapo Benki ya NMB iliwasaidia kukabiliana na changamoto hiyo kwa kuwapa mikopo ambayo iliwasaidia kuinuka kiuchumi.
Ofisa Maendeleo ya Jamii wa mji wa Kibaha, Novman Gimbi, aliwasihi vijana kuchangamkia fursa zilizopo kwa kufika katika ofisi za halmashauri, ili waweze kunufaika na mikopo inayotolewa endapo kijana atakuwa amejiunga na Chama cha Akiba na Mikopo (Saccos).
Katika hafla hiyo zaidi ya wateja 20 walizawadiwa zawadi mbalimbali zikiwemo simu za mikononi, vocha na zawadi nyingine
Chanzo;Tanzania daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Pwani Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa