WANAFUNZI 200 wamekuwa wakilazimika kubanana kwenye darasa moja wakati
wa vipindi vya masomo katika shule ya Msingi Kongowe iliyopo halmashauri
ya mji Kibaha kutokana na shule hiyo kukabiliwa na uhaba wa vyumba vya
madarasa.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Beatus Lingumbuka ameweka wazi hali hiyo
wakati akielezea changamoto na mafanikio ya shule hiyo kwa waandishi wa
habari waliofika hapo kujua sababu zinazopelekea idadi hiyo kubwa ya
watoto kuminyana kwenye darasa moja.
Amesema shule hiyo ina wanafunzi 1,502 kati yao wa kitengo cha
watoto wenye ulemavu ni 42 idadi ambayo ni kubwa ikilinganishwa na
madarasa yaliyopo hivi sasa.
Mwalimu mkuu Lingumbuka amesema madarasa yaliyopo ni kumi lakini
yanayotumika ni saba tu huku matatu yakiwa ni chakavu kwa miundombinu
yake na hivyo kuifanya shule hiyo kuwa upungufu wa madarasa 14 kwa sasa
ambayo ndiyo yatakayokidhi mahitaji kulingana na idadi ya wanafunzi
waliopo hapo.
Nae Diwani wa Kata ya Kongowe, ambae pia ni makamu mwenyekiti
halmashauri ya mji Kibaha, Sloom Bagumeshi amesema atahakikisha anavalia
njuga suala hilo ili kupunguza tatizo hilo na pia atazungumza na wapiga
kura wake wachangie nguvu kazi na fedha huku akiitaka halmashauri na
wadau wengine kushirikiana kuchangia ujenzi wa madarasa walau matatu ili
kupunguza hali hiyo mapema.
Hata hivyo, kuhusu uwepo wa idadi kubwa ya wanafunzi shuleni hapo ,
Bagumeshi amekiri ipo kinyume na miongozo ya Serikali inayoelekeza
kuwepo wanafunzi 750 kwa shule moja hivyo inatakiwa kugawanywa na kuwa
shule mbili kwani bila ya hivyo msongamano wa wanafunzi darasani
hautakoma mapema.
Home »
» WANAFUNZI 200 WASOMA KWENYE CHUMBA KIMOJA CHA DARASA
0 comments:
Post a Comment