HIVI karibuni, Korea Kusini ilitoa mafunzo ya siku kumi kwa viongozi mbalimbali kutoka nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania, msafara ambao uliongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Mercy Sila.
Pamoja na mambo mengine, lengo la mafunzo hayo yalikuwa kufanya tathmini kuhusu namna vijiji viwili vya Njia Nne na Mfuru Mwambao, vyote vya Mkuranga, mkoa wa Pwani vitakavyoweza kujiendesha bila kutegemea tena msaada kutoka asasi ya Saemaul Undong (SMU) (kampeni ya maendeleo vijijini) ambayo imekuwa ikivisaidia kwa miaka mitano iliyopita.
Takribani nchi 22 ikiwemo Tanzania, zilituma idadi ya viongozi 72 katika mkutano huo, ambao hatimaye majumuisho yake yaliwaridhisha pasipo shaka yoyote wafadhili hao wa Korea kwamba, kuna uwezekano mkubwa wa nchi hizo kuweza kujitegemea kwa kuiendesha miradi waliyoanzishiwa bila misaada tena ya kutoka Korea Kusini.
Katika ziara ile, yapo mengi yaliyojiri likiwemo suala la mataifa mbalimbali kuwasilisha mipango na mikakati endelevu inayoonesha namna watakavyopiga hatua kwa miaka mitano na zaidi ijayo. Kazi iliyobaki kwa washiriki ni kuyaingiza katika matendo mafunzo waliyoyapata na kuondokana na utegemezi wa kusubiri maendeleo ya kimiujiza hasa katika zama za maendeleo endelevu katika ulimwengu wa kisasa wa Sayansi na Teknolojia.
Baada ya kurejea nchini, nimefanya mahojiano na Mkuu huyo wa Wilaya ya Mkuranga pamoja na viongozi walioambatana naye nchini humo, ili kujua kipi walichojifunza na mikakati gani waliyokuja nayo katika kuyasogeza mbele maisha ya wananchi waliowatuma Korea.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya, Mercy Silla anasema, Tanzania kama zilivyo nchi nyingine, ina mambo mengi ya kujifunza kutoka nchini Korea Kusini kutokana na kile anachoeleza kwamba nchi hiyo ilikuwa karibu sawa na Tanzania kimaendeleo lakini kwa sasa, kutokana na mabadiliko makubwa ya kifikra, nchi hiyo imepiga hatua kubwa kimaendeleo na kuiacha Tanzania nyuma.
Sila anasema, kwa muda ambao wamekuwa nchini humo, wamejifunza siri za mafanikio za taifa hilo ambalo limo kwenye mataifa yanayokua kwa kasi kiuchumi duniani na hivyo kuwa nchi ya 13. Anasema, wananchi wa Korea Kusini kwa miaka mingi wamejifunza kufanya kazi kwa bidii, kushirikiana na kujitolea kwa ajili ya maendeleo yao wenyewe, jambo lililosababisha mabadiliko makubwa ya kiuchumi na kijamii miongoni mwao kuanzia vijijini hadi mijini.
Kwa mujibu wa Mkuu huo wa Wilaya, falsafa ya Korea Kusini kuhusu dira ya maendeleo, inafanana na sera za Ujamaa na Kujitegemea, sera ambayo iliasisiwa na Rais wa kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere, jambo linaloonesha kama mpango huo usingehujumiwa na wachache basi pengine Tanzania ingepiga hatua kimaendeleo kuliko ilivyo sasa.
“Kutokana na falsafa hiyo ya Ujamaa na Kujitegemea, Korea ya Kusini kupitia kiongozi wake wa wakati huo Park Chung Hee, alithubutu kufanya maamuzi magumu ikiwa ni pamoja na kuwapa wananchi wake dira na maono makubwa ambayo yaliwasukuma kutumia nguvu zao kwa lengo la kufanya mapinduzi makubwa ndani ya nchi yao,” anasema.
Anafafanua kwamba kuhusu suala la mazingira, misitu na maliasili kwa ujumla, tangu mapema Rais Park alivyokuwa anaweka misingi ya Taifa hilo, alisisitiza kuwa kila eneo lililo wazi hata kama liko juu ya jiwe au mwamba, lilitakiwa kupandwa miti kwa wingi, hususan wakati wa msimu wa masika jambo ambalo limekuwa linaendelezwa na kusimamiwa hadi leo.
Kwa upande wa vijiji vya Korea, Sila anasema vimeendelezwa kiasi kwamba, kwa mtu anayetokea Afrika ni vigumu kuvitofautisha na mijini na kuongeza kwamba uwiano wa ongezeko la watu mijini na vijijini ni asilimia hamsini kwa hamsini jambo linaloweka uwiano wa kimaendeleo kati ya mijini na vijijini.
Mwajuma Kingwande ni Diwani wa Kata ya Njia nne Mkuranga, Pwani ambaye alikuwa katika msafara huo. Kwa upande wake anasema, kinachofanyika Korea kwa sasa, sio kitu kigeni kwa harakati za maendeleo ya nchi yetu na kuongeza kuwa, kampeni za vijiji vya Ujamaa vilikwishaanzishwa hapa nchini hivyo mafunzo waliyoyapata yamewaamsha kutilia mkazo masuala hayo.
“Jukumu letu kubwa hasa mimi binafsi katika Kata ya Njia Nne, tumelenga kuanza kuhimizana kila mtu kuhakikisha kuwa tunajipanga zaidi kwa ajili ya kuinua maisha ya wananchi angalau kwa kiwango ambacho wanaweza kujiona wako mahali fulani tofauti na pale walipo kwa sasa kutokana na ugumu wa maisha,” anasema.
Diwani Mwajuma anafafanua kwamba Kata ya Njia Nne ambayo ina jumla ya vijiji vitano, inatarajiwa kukua kiuchumi muda mfupi ujao baada ya kujengewa uwezo na kwamba katika hatua za wali yeye kama kiongozi, amelenga kuitisha kikao na Baraza la Maendeleo la Kata mapema kadiri iwezekanavyo.
Anafafanua kwamba pamoja na mambo mengine lengo la mkutano huo ni kutoa mwongozo, dira na mtazamo wa pamoja kwa miaka mitano ijayo ili ikiwezekana, Kata hiyo iwe ya mfano katika miradi inayofadhiliwa na SMU ya Korea ambayo ni nyumba bora, mashamba ya pamoja, uimarishaji wa miundombinu ya barabara n.k.
“Pamoja na changamoto mbalimbali hapa kwetu, ninashukuru kwa kiasi fulani tumepiga hatua zinazoonekana ila hatujafika mahali pale tunapopataka, ndiyo maana natamani sana kata yangu kwanza iwe ya mfano kupitia vijiji vyake vyote vitano na baadaye kuifikisha miradi hiyo katika kata nyingine za jirani na mikoa mingine nchini,” anasema Diwani huyo.
Mwinjilisti Maiko Madafu, Katibu wa kikundi cha uzalishaji mali cha ‘Saemaul Undong’ cha kijiji cha Mfuru Mwambao, yeye anashangazwa na baadhi ya vijana hapa nchini kuwa mbali na masuala ya miradi ya kujitolea, tofauti sana na wenzetu wa Korea Kusini alikokuwa na kujionea.
Anasema, kutoka na mwamko aliouona nchini humo wa vijana kuwa na moyo wa kujitolea, kuna kazi kubwa sana nchini Tanzania kugeuza fikra za vijana wa nyumbani wakubali kujitolea wanapotakiwa kufanya hivyo na kuondokana na mawazo mgando kwamba kilimo ni kazi ya wazee na badala yake, wajihusishe nacho na wajibidiishe katika kilimo na kazi za mikono kwa ujumla.
Maiko anafafanua kwamba kupambana na umasikini kivitendo ni suala ambalo linahitaji nguvu ya pamoja kwa ushiriki wa kila rika lenye uwezo wa kufanya kazi wakiwemo vijana, jambo litakalochangia kwa kiasi kikubwa kupunguza umasikini na kuongeza ajira nchini. Kwa mujibu wa katibu huyo, kitendo cha baadhi ya vijana nchini kujitenga katika suala zima la kilimo si dalili nzuri kiuchumi na kwamba ni dalili mbaya kwa kwa uchumi endelevu.
“Kwa njia moja ama nyingine, ugumu huo hujitokeza kwa kusababishwa na baadhi ya viongozi kutokuwashirikisha vijana katika hatua za awali, jambo linalowasababisha waendelee kuwa pembeni lakini hata hivyo uzoefu unaonesha walio wengi huwa wanajitenga wenyewe,” anasema.
“Vijana wa Korea wana bidii, umakini na nidhamu ya kipekee katika kazi za kujitolea ikilinganishwa na Tanzania, suala linalohitaji kubadilisha mtazamo na mawazo kwa vijana hao na jamii kwa ujumla,” anasema. Kiongozi huyo anawashauri viongozi wa SMU nchini wasibweteke na kiasi cha maendeleo ambayo wamepata mpaka sasa, na badala yake wawe na maono na wayasimamie ili mabadiliko hayo yapeleke maendeleo hata kwa vijiji vingine.
Katika mipango yake ya mwaka huu, Ofisi ya Halmashauri ya Mkuranga kwa kushirikiana na SMU, wanatarajia kujenga Daraja la Nyamihimbo litakalokuwa chachu ya maendeleo katika kata hiyo na kata jirani SMU Korea mpaka sasa imeshasaidia kata ya Njia Nne Mkuranga ukarabati wa soko, ujenzi wa fremu 10 za maduka, kisima cha maji, ukumbi wa mikutano, duka la pembejeo za kilimo na vifaa vya ujenzi la kijiji, miradi ambayo itakuza kipato cha kaya kadhaa na wilaya ya Mkuranga kwa ujumla.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment