WANANCHI wametahadharishwa kuacha tabia ya kuishi kwa mazoea hasa katika
masuala ya mabadiliko ya hali ya hewa na badala yake waishi kulingana na
mazingira ya hali ya hewa wanayotangaziwa na Mamlaka husika kwani kwa kuzitumia taarifa hizo vizuri
kutasaidia kuongeza uzalishaji katika maeneo mengi ya sekta za uchumi na
kupunguza vifo vitokanavyo na machafuko ya baharini na ziwani.
Mkuu wa mkoa wa Pwani Mwantumu
Mahiza ametoa tahadhari hiyo jana wakati akifungua warsha ya Wahariri wa vyombo
mbalimbali vya habari nchini kuhusu huduma za hali ya hewa na nafasi ya vyombo
hivyo katika sekta ya hali ya hewa mkutano ambao ulifanyika mjini Kibaha.
Mahiza amesema Watanzania wengi
wamekuwa na tabia ya kukurupuka tu kwa imani ya Mungu ndiye ajuaye na kujiendea
katika shughuli zao ikiwemo za uvuvi,usafiri wa baharini na ziwani,kilimo hasa
aina ya mazao yanayostahili kuyapanda wakati huo bila ya kufatilia hali ya hewa
ya wakati huo inaelekeza nini,na kwa wakati gani.
Amesema ukurupukaji wa aina hiyo
imekuwa ikichangia kushuka uchumi na pia kuleta madhara mbalimbali ikiwemo vifo
vya majini na kisha jamii kuilaumu Serikali wakati makosa wanayo wenyewe kwa
utamaduni wao wa kutokuwa na tabia ya kufatilia matangazo ya mabadiliko ya hali
ya hewa yanayotolewa kila siku na Idara husika katika vyombo vya habari.
Kutokana na hali hiyo, Mkuu huyo wa
mkoa ameitaka Mamlaka ya hali ya hewa nchini wakae na Waziri wa Uchukuzi
watengeneze muswada mdogo wapeleke Bungeni waangalie namna ya kuwabana watu
ambao hupuuzia matangazo ya mabadiliko ya hali ya hewa na kusababisha madhara.
Awali Mkurugenzi mkuu wa Mamlaka wa
hali ya hewa nchini(TMA) Dkt Agnes Kijazi amesema pamoja na ushirikiano uliopo
na vyombo vya habari pia imekuwepo changamoto ya lugha inayotumika kutoeleweka
vizuri pamoja na baadhi ya vyombo vya habari kutoa taarifa ambazo hazijatolewa
na Mamlaka hiyo.
Dkt Kijazi amesema hali hiyo imekuwa
ikiwasababishia Mamlaka hiyo kupokea maswali mengi toka kwa wananchi pale
ambapo utabiri huo unapokuwa si sahihi na kutofautiana sana na utabiri
unaotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa.
Amesema kutokana na changamoto hiyo
ndiyo maana Mamlaka ya hali ya hewa imeandaa warsha hiyo kwa Wahariri hao ili
kwa pamoja wapate fursa ya kujadiliana na kukubaliana njia bora zaidi
itakayowezesha taarifa sahihi zitolewazo na Mamlaka ya Hali ya Hewa zinawafikia
walengwa kwa wakati.
0 comments:
Post a Comment