Home » » BAGAMOYO WAFIDIWE KWA KUJENGEWA NYUMBA- JK

BAGAMOYO WAFIDIWE KWA KUJENGEWA NYUMBA- JK



 Ni katika kupisha ujenzi wa bandari

Rais Jakaya Kikwete, akitembelea mabanda mbalimbali yaliyopo kwenye Maonyesho ya 37 ya Biashara ya Kimataifa yanayofanyika katika Viwanja vya Julius Nyerere jijini Dar es Salaam jana.
Rais Jakaya Kikwete ametangaza neema kwa wakazi wa Bagamoyo ambao watapisha ujenzi wa bandari kubwa inayokusudiwa kujengwa na China kwa kuagiza wajengewe nyumba kama fidia ili 'wasiyumbe kiuchumi.'
Rais Kikwete alitangaza neema hiyo jana jijini Dar es Salaam alipotembelea Maonyesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) maarufu kama Sabasaba yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, barabara ya Kilwa.

Rais Kikwete alitoa agizo hilo kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ukanda wa Uwekezaji (EPZA), Dk. Adelhem Meru, alipotembelea banda la mamlaka hiyo.

"Hakikisha mnawasiliana na Bandari jinsi gani ya kuwalipa fidia wakazi wa Bagamoyo mtakaowahamisha kwa kuwajengea nyumba sehemu nyingine ili wakazi hao wasiyumbe kiuchumi," aliagiza Rais Kikwete.

Ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo itakayofanywa kwa mkopo wa zaidi ya Sh. trilioni 16 (Dola bilioni 10 za Marekani) unagharimiwa asilimia 100 na serikali ya China.

Hii ni kufuatia ziara ya Rais wa China, Xi Jinping, nchini aliyoifanya Machi 24 na 25, mwaka huu baada ya kusaini mikataba 16 yeye na mwenyeji wake, Rais Kikwete kwa ajili ya miradi ya maendeleo Tanzania Bara na mikataba mitatu kwa Zanzibar wakati wa ziara yake ya kiserikali nchini.

Ujenzi huo umepangwa kumalizika mwaka 2017 na utafanywa na kampuni ya Merchants Holdings kutoka China na itakuwa na uwezo mkubwa zaidi kuliko Bandari Dar es Salaam.

Awali, Dk. Meru alisema tayari ekari 230,000 zimeshatengwa kwa ajili ya ujenzi wa bandari hiyo.

Alisema mpaka sasa ekari 25,000 zimeshalipiwa fidia kutoka kwa wananchi na ifikapo Septemba, mwaka huu ujenzi wa bandari hiyo utaanza.

Aidha, Dk. Meru alisema Serikali kwa kushirikiana na China inatarajia kujenga mradi wa viwanda vikubwa vya biashara utakachogharimu Sh. bilioni 600 eneo la Kurasini jijini Dar es Salaam.

Dk. Meru alisema pindi ujenzi wa mradi huo utakapokamilika kitakuwa ni kituo kikubwa cha biashara cha Afrika Mashariki.

Alisema zoezi linaloendelea kwa sasa ni ulipaji wa fidia kwa wakazi wanaoishi katika eneo hilo.

Alisema eneo hilo lina ukubwa wa ekari 60 na kueleza kuwa Serikali ya Tanzania imetoa eneo na Serikali ya China itagharimia ujenzi wote wa mradi huo wa viwanda.

Alisema Sh. bilioni 90 zinahitajika katika ulipaji wa fidia kwa wakazi hao na mpaka sasa wamekwisha kupata Sh. bilioni 25 kwa ajili wa kazi hiyo.

Alisema pindi mradi huo utakapokamilika utaleta ajira kwa wananchi pamoja na urahisi wa upatikanaji wa bidhaa kwa wananchi hapa nchini.

“Kwa sasa ulipaji wa fidia umeshaanza na ujenzi utaanza muda wowote baada ya ulipaji wa fidia kukamilika, lakini mradi huu utaleta faida kubwa kwa wafanyabishara hapa nchini,” alisema Dk. Meru.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Pwani Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa