Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
MKUU wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo amesema wafanyabiashara
watakaokaidi kufanya usafi kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi watapigwa
faini ya Sh 50,000 papo kwa hapo.
Aliyasema hayo mjini Kibaha mara baada ya kumaliza kufanya usafi
katika maeneo mbalimbali ya mji wa Kibaha wakati wa kutekeleza agizo la
Rais Dk John Magufuli la kila mkoa kufanya usafi kila mwezi.
Alitoa kauli hiyo kufuatia baadhi ya wafanyabiashara kufungua
biashara zao na kutofanya usafi licha ya kutangaziwa kuwa wanapaswa
kufunga biashara zao kwa saa kadhaa kwa ajili ya kufanya usafi wa maeneo
yao.
“Inashangaza kuona baadhi ya watu wanakaidi agizo la viongozi wao kwa
kutofanya usafi wa maeneo yao huku wakiendelea kufanya biashara kwenye
mazingira machafu,” alisema Ndikilo.
Alisema usafi ni suala la kila mtu na si kwa baadhi ya watu, hivyo
kila mkazi na mfanyabiashara wa Pwani anapaswa kutenga muda kwa ajili ya
usafi wa mazingira.
Aidha, alisema mbali ya kupigwa faini za papo hapo pia watafikishwa
kwenye vyombo vya sheria ikiwa ni pamoja na kupelekwa mahakamani kwa
kukaidi agizo la Rais.
“Mbali ya kufanya usafi wa nje hatua inayofuata ni kufanya usafi wa
ndani kama vile kwenye maeneo ya mahoteli, migahawa, nyumba za kulala
wageni na sehemu nyingine za kutoa huduma kwa watu,” alisema Ndikilo.
Aliwasisitiza wananchi kujenga tabia ya kufanya usafi ili kukabiliana
na magonjwa mbalimbali yatokanayo na uchafu hasa yale ya mlipuko
kikiwamo kipindupindu ambacho kwa Pwani kimedhibitiwa, kwani kwa sasa
hakuna mgonjwa hata mmoja.
CHANZO ; HABARI LEO.
0 comments:
Post a Comment