Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Na Lilian Lundo - Maelezo
Wananchi kata
ya Kisaki, wilaya ya Morogoro Vijijini kunufaika na nishati ya jotoardhi
inayotokana na chanzo cha maji ya moto yaliyoko katika kata hiyo.
Akiongea na kamati ya maendeleo ya kata ya Kisaki
leo, Mkurugenzi Mhandisi Kato Kabaka wa Kampuni ya Uendelezaji wa Jotoardhi
Tanzania aliiambia kamati hiyo kuwa, Kisaki ni mojawapo ya Kata ambazo
zitanufaika na nishati ya umeme itokanayo na jotoardhi.
“Jotoardhi ni nishati ya gharama nafuu ambayo ni
jadidifu, yaweza kuvunwa kwa miaka mingi bila kuisha tofauti na nishati zingine
zinazo athiriwa na mabadiliko ya tabia ya nchi, hivyo mitambo yake itakapowashwa haitazima labda pale tu patapohitajika
marekebisho ya kiufundi.” Alisema Bwana Kato.
Bwana Kato aliongezea kwa kusema kuwa, Jotoardhi ina
faida mbadala mbali na nishati ya umeme.
Faida hizo zinatokana na joto na kemikali ambazo zinapatikana katika
majimoto ambayo hutumika kukausha mazao,
kuogeshea mifugo, kutumika katika kilimo, ufugaji wa samaki pamoja na kutumika
katika mabwawa ya kuogolea kwenye mahoteli ya kitalii na hata majumbani.
Kupitia kikao hiko Bwana Kato aliiomba kamati hiyo
kuukubali mradi huo ili Kampuni ya Uendelezaji wa Jotoardhi Tanzania iweze kuendelea
na utafiti wa jotoardhi katika kata ya Kisaki hatimaye wananchi waweze
kunufaika na nishati hiyo pindi mradi huo utakapokamilika.
Kamati imeupokea mradi huo, na kusema umekuja wakati
muafaka kwani kata ya Kisaki haijafikiwa na umeme. Hivyo mradi huo
utawanufaisha kwa kuwaletea umeme katika vijiji vyao.
Jotoardhi ni mojawapo ya chanzo cha nishati
kinachotumia joto lililopo katika gamba la dunia. Joto hili linatokana na
mchakato wa ndani ya tufe la dunia na kiasi kidogo jotojua linapokelewa kwenye
uso wa dunia.
Maeneo mengine yenye viashiria vya jotoardhi ni Ziwa
Manyara, Kreta ya Ngorongoro, Utete (Pwani), Luhoi (Pwani) Songwe (Mbeya),
Ngozi, Rukwa, Kilambo, Mampulo, Ibadakuli(Shinyanga), Mtagata (Kagera), Dodoma,
Singida na Tanga.
Serikali ilianzisha kampuni hii ya kuendeleza
nishati ya jotoardhi (Tanzania Geothermal Development Company Limited -TGDC)
mwaka 2013 ili kufanya tafiti za kina na kuendeleza kwa haraka nishati ya
jotoardhi nchini ili kufikia mwaka 2020 taifa liwe na megawati 200 zinazozalishwa
kwa jotoardhi.
0 comments:
Post a Comment