Home » » MAHIZA AZISHUKIA ASASI ZA UKIMWI

MAHIZA AZISHUKIA ASASI ZA UKIMWI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

MKUU wa Mkoa wa Pwani, Mwantum Mahiza, amesema anashangazwa na uwepo wa asasi nyingi zinazotoa elimu namna ya kuepuka maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi huku takwimu za maambukizi zikiendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka.
Amesema anashindwa kuelewa kazi inayofanywa na asasi hizo, kwani bado kuna maambukizi mapya mkoani hapa huku zikiendelea kupata fedha kutoka kwa wafadhili kwa ajili ya kutoa elimu hiyo.
Mahiza, alisema ni wakati sasa kila asasi kuweka wazi kazi inayofanya na maeneo yake ili ufuatiliaji ufanyike, badala ya kuendelea kuwa na mlundikano wa asasi ambazo kazi zinazofanywa taarifa zake hazifiki kwenye Halmashauri.
Aidha, Mahiza alizionya asasi zisizo za serikali zinazowatumia watoto yatima kama sehemu ya kujipatia mitaji kutoka kwa wafadhili, kuacha tabia hiyo na atakayebainika hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
Mkuu huyo wa Mkoa, alitoa kauli hizo kwa nyakati tofauti Mjini Kibaha katika mkutano wa mashirika yasiyo ya kiserikali uliokuwa umeandaliwa chini ya ofisi ya Idara ya Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Pwani, kupitia ofisa wake Asha Itelewe, ambako lengo ilikuwa kujadili changamoto zilizopo.
Mahiza, alisema zipo asasi nyingi ambazo zimekuwa zikitumia watoto yatima kupata fedha kwa wafadhili na wanapofanikiwa, watoto hao wanaachwa wakiendelea na maisha magumu na wao kufanyakazi zenye maslahi yao binafsi.
Alisema kuwa, jambo la msingi ni kuhakikisha wanafanyakazi ya kutafuta fedha, ambazo kwa kiasi kikubwa zitawaelimisha ndugu ili wajue namna ya kuwatunza watoto hao kuliko kufanya mambo ambayo yanadhalilisha binadamu wenzao.
Mkutano huo ulishirikisha asasi kutoka Wilaya za Mkuranga, Rufiji, Kisarawe, Kibaha na Bagamoyo, nyingi zikiwa zimejikita kufanya kazi katika masuala ya ukimwi, yatima, mazingira, jinsia na wazee.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Pwani Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa