Home » » MADIWANI KYELA WAJINOA USAFI WA MAZINGIRA KIBAHA

MADIWANI KYELA WAJINOA USAFI WA MAZINGIRA KIBAHA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

MADIWANI wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyela mkoani Mbeya wamefanya ziara ya mafunzo kwa kuitembelea Halmashauri ya Mji Kibaha kwa lengo la kujifunza jinsi ya uboreshaji na usafi wa mazingira.
Akizungumza katika kikao cha mafunzo hayo yaliyofanyika ukumbi wa Halmashauri ya Mji Kibaha yakiwakutanisha Madiwani na wakuu wa idara kwa nia ya kupeana maarifa, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kyela, Gabriel Kipija, alisema hawakuja Kibaha kimakosa bali kutokana na ukweli wa mambo kuwa, Kibaha ni safi.
Akiwakaribisha, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Kibaha, Sloom Bagumesh, aliwapongeza Madiwani na watendaji kutoka Kyela kwa kuja kujifunza na wamefanya chaguo sahihi, kwani si jambo la kubeza kuwa  miaka ya hivi karibu Kibaha imefanya vema katika nyanja za usafi wa mazingira.
Akisoma taarifa ya namna anavyokabiliana na usafi wa mazingira katika Mji wa Kibaha, Mkuu wa idara hiyo, Tumaini Kayila, alisema pamoja na kufanya mikutano na wananchi kutoa elimu namna ya utunzaji sahihi wa mazingira kuanzia ngazi ya mtaa, vimeundwa vikundi 13 vinavyofanya kazi ya uzoaji taka majumbani.
Aidha, Halmashauri imekuwa ikiwapa vitendea kazi kama matoroli, baiskeli za magurudumu matatu ‘guta’, na pikipiki za magurudumu matatu kwa ajili ya kusafirishia taka kutoka sehemu za pembezoni na kuzikusanya kwenye vizimba.
“…dampo letu lipo nje ya Mji, vikundi hivi hukusanya taka toka sehemu mbalimbali na kuziweke kwenye vizimba. Baada ya hapo magari yetu mawili yenye uwezo wa tani 7 huzisafirisha mpaka dampo ambapo kwa siku tuna uwezo wa kusafirisha tani 14,” alisema.
Mwaka wa fedha 2013/2014, Kibaha imeshika nafasi ya tatu kwa utunzaji na usafi wa mazingira ikiwa nyuma ya Jiji la Mwanza na Manispaa ya Moshi.
Ziara hiyo iliyokuwa na ujumbe wa watu 37 wakiwemo madiwani 27 na watendaji 10 pamoja na mambo mengine, ililenga pia kujifunza namna ya upimaji na uuzaji wa viwanja na ukusanyaji wa mapato kwa njia ya Ki-elektoniki hasa kwa kutumia Max Malipo.
Chanzo:Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Pwani Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa