Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Wanamichezo wanaoshiriki michuano ya Umoja wa Shule za
Sekondari Tanzania (Umisseta) wametakiwa kuzingatia nidhamu, umoja na
mshikamano ndani na nje ya uwanja katika michuano hiyo iliyoanza jana
kwenye viwanja vya Shirika la Elimu mjini hapa.
Mratibu wa michezo wa Ofisi ya Waziri Mkuu
(Tamisemi), Mohamed Kiganja alitoa rai hiyo jana wakati wa mazoezi ya
asubuhi ya timu shiriki uwanjani hapo.
Kiganja alisema wanamichezo wote wanapaswa
kuzingatia kaulimbiu ya mashindano hayo, ambayo ni Kudumisha Michezo,
Amani na Upendo.
“Michezo ni afya, ajira na furaha. Wanamichezo
mlioko hapa ndiyo zao la timu za taifa za baadaye. Lakini mtafanikiwa
kufika huko endapo tu mtazingatia nidhamu na kuwa wamoja,” alisema.
Alisema kuwa ufunguzi rasmi utafanyika leo mchana na mgeni rasmi atakuwa Naibu Waziri Kassim Majaliwa.
Alisema kabla ya zoezi la ufunguzi kutakuwa na
mechi za makundi katika soka, netiboli, kikapu, wavu na mpira wa mikono
zitakazochezwa asubuhi uwanjani hapo.
Wanamichezo 1,561 kutoka kanda ya Dar es Salaam,
Kati, Ziwa, Ziwa Magharibi, Mashariki, Magharibi, Kusini, Kaskazini,
Kaskazini Magharibi, Kaskazini Mashariki, Nyanda za Juu na Nyanda za Juu
Kusini watachuana kwenye michezo saba tofauti kwa wiki mbili kuanzia
jana kabla ya kufanyika ile ya shule za msingi (Umitashumta) uwanjani
hapo.
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment