Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Muonekano wa mji wa bagamoyo utakavyokuwa baada ya kukamilika kwa mradi wa uwekezaji wa bandari. Picha na Maktaba
Mradi wa Bandari ya Mbegani – Bagamoyo, mkoani Pwani ndiyo
mradi mkubwa wa uwekezaji nchini utakaoifanya wilaya hiyo kuwa na
mwonekano mpya.
Aidha, kukamilika kwa mradi huo kunatarajiwa
kuliingizia taifa kiasi kikubwa cha fedha na kuzalisha fursa nyingine
nyingi za kiuchumi.
Serikali ya Tanzania na Serikali ya China kupitia
Kampuni ya China ya Merchants, ziliingia mkataba wa makubaliano ya
ujenzi wa bandari hiyo kwa utaratibu wa ubia kati ya sekta ya Umma na
sekta Binafsi (PPP).
Ujenzi huo ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo, ambao hufanyika kwa kipindi cha miaka mitano mitano.
Kupitia mradi huo, vipaumbele katika kipindi cha
kwanza kuanzia 2011/12 – 2015/16 ni kufungua fursa za kiuchumi na
uwekezaji katika sekta za nishati, usafirishaji na Tehama.
Akiwasilisha hotuba ya bajeti ya Wizara ya Viwanda
na Biashara kwa mwaka 2014/15 bungeni hivi karibuni, Waziri wa wizara
hiyo, Dk Abdallah Kigoda alisema kuwa wizara yake ina mpango wa kulipa
fidia kwa wakazi wa maeneo yaliyofanyiwa uthamini Bagamoyo na maeneo
mengine nchini.
Alieleza kuwa Mradi wa Bandari unahusisha
Maendeleo ya Maeneo Maalumu ya Kiuchumi (SEZ) katika eneo lenye ukubwa
wa hekta 9,080 litakalojumuisha shughuli za ujenzi wa barabara, mitandao
ya mawasiliano, mifumo ya maji na umeme.
Shughuli zitakazofanyika katika eneo hilo ni
pamoja na viwanda, vituo vya biashara, vivutio vya utalii, Teknolojia ya
Habari na Mawasiliano, Huduma ya Makazi, Taasisi za Fedha na Makao
Makuu ya Mkoa.
Alisema kukamilika kwa ujenzi wa Bandari ya
Mbegani Bagamoyo kutasaidia kupunguza foleni kwa kiasi kikubwa katika
Bandari ya Dar es Salaam na kuifanya Tanzania kuwa na bandari kubwa na
ya kisasa katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Dk Kigoda alisema wataanza uendelezaji wa
miundombinu ya msingi kwa Maeneo Maalumu ya Uzalishaji kwa Mauzo ya Nje
(EPZ) na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi (SEZ) yaliyolipiwa fidia kama vile
Bagamoyo SEZ.
Aliongeza kuwa kwa mwaka huu wa fedha, Serikali
imetenga Sh7 bilioni kwa ajili ya kumalizia ulipaji fidia katika eneo la
Bagamoyo.
Alifafanua kwamba mwaka 2013/14, kampuni 31
zilipewa leseni za kujenga viwanda chini ya Mamlaka ya EPZ na tayari
kampuni nane zimeanza uzalishaji. Kampuni hizo zinatarajiwa kuwekeza
mtaji wa jumla ya Dola za Marekani 485 milioni na kuajiri watu 10,276.
Idadi hiyo inafanya kampuni zinazofanya uzalishaji chini ya EPZ
na SEZ kufikia 98, huku jumla ya mtaji uliowekezwa ukifikia Dola 1.5
bilioni, pamoja na ajira kufikia watu 27,000.
Hata hivyo, Dk Kigoda alisema hatua za awali za uendelezaji wa Bagamoyo SEZ yenye ukubwa wa hekta 9,000 umeshaanza.
Alibainisha kuwa kati ya hekta 9,000 hizo, hekta
6500 zitaendelezwa na Mamlaka ya EPZ na zilizobaki zitaendelezwa na
Kampuni ya Kichina ya Biashara (CMHI).
Alisema wizara yake ikishirikiana na Ofisi ya
Waziri Mkuu, inajadiliana na Kampuni ya CMHI ili kujenga bandari ya
kisasa na eneo la viwanda katika eneo la hekta 2,500 ndani ya eneo la
Bagamoyo SEZ.
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment