MHE. RIDHIWANI KIKWETE AONGOZA MAMIA YA WANANCHI WALIOJIAJIRI KUJIUNGA NA KUJIWEKEA AKIBA NSSF


*Ni katika muendelezo wa kampeni ya elimu kwa umma kuhusu Skimu ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii kwa Wananchi Waliojiajiri Chalinze mkoani Pwani 

*NSSF yaahidi kufikisha elimu ya hifadhi skimu kwa wananchi wengi zaidi

Na MWANDISHI WETU, PWANI

Waziri wa Nchi,  Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Ridhiwani Kikwete amewaongoza mamia ya wananchi wa Chalinze mkoani Pwani, katika muendelezo wa elimu kwa umma kuhusu Skimu ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii kwa Wananchi Waliojiajiri yenye jina la kampeni  "NSSF STAA WA MCHEZO".

Akizungumza na wananchi waliojiajiri, mwishoni mwa wiki iliyofanyika Chalinze mkoani Pwani, Mhe. Ridhiwani ameipongeza NSSF kwa kuja na skimu hiyo ambayo itakuwa mkombozi kwa wananchi waliojiajiri ili kunufaika na mafao ya muda mfupi yakiwemo ya matibabu na mafao ya muda mrefu ambayo ni uzeeni.

Mhe. Ridhiwani amewataka wananchi waendelee kujiunga  na kujiwekea akiba kwa ajili ya maisha yao ya sasa na ya baadaye. "Unapojiunga na skimu hii pale unapougua utanufaika na matibabu, ukipata ulemavu utanufaika na mafao ya ulemavu, ukiwa mzee utanufaika na mafao ya uzeeni hivyo ni muhimu kila mwananchi kuchangamkia fursa hii, kwa kujiweka akiba," amesema Mhe. Ridhiwani.

Amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maoni na miongozo yake ambapo kupitia Serikali ya awamu ya sita, wananchi waliojiajiri wanajiwekea akiba NSSF na kunufaika na mafao na huduma nyingine.

"Mpango ulioletwa na NSSF ni kwa ajili ya leo na kesho yako, kwani itafika siku nguvu ya kufanyakazi zitapungua na hapo ndipo NSSF itachukua nafasi ya kuwa Staa wa Mchezo kwa kulipa mafao ya pensheni ya uzee na matibabu," amesema Mhe. Ridhiwani.

Amesema NSSF imeweka utaratibu nzuri wa kujiunga na kuchangia kidogo kidogo kwa siku buku buku, hivyo amewataka wananchi kuendelea kujiunga na kuchangia ili kunufaika na mafao pamoja na huduma nyingine zinazotolewa na Mfuko.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. Masha Mshomba, Mkurugenzi wa Uendeshaji, Bw. Omary Mziya, amesema hifadhi skimu inawahusu wananchi waliojiajiri katika maeneo mbalimbali ya kiuchumi na kuwa inaenda kufungua milango kwa wananchi kunufaika na mafao mbalimbali yanayotolewa na NSSF yakiwemo na matibabu. 

Awali,  Mwenyekiti wa Halmashauri ya Chalinze, Mhe. Hassan Mwinyikondo ameipongeza NSSF kwa kuja na skimu hiyo ambayo itakuwa mkombozi wa wananchi waliojiajiri.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Mhe. Shaibu Ndemanga amemewahakikishia wananchi wa Chalinze na Bagamoyo kuwa mpango huo ni mkombozi kwa wananchi hususani watakapoishiwa nguvu ya kufanyakazi, kwani watapata mafao kutoka NSSF.



WANANCHI WALIOJIAJIRI CHALINZE WACHANGAMKIA KUWA MASTAA WA MCHEZO WA NSSF


Tayari timu ya NSSF ipo mtaani katika Soko la Bwilingu na maeneo mengine ya Halmashauri ya Chalinze mkoani Pwani kwa ajili ya kutoa elimu ya hifadhi ya jamii, kwa wananchi waliojiajiri ambapo mwamko wa wananchi kujiunga na kujiwekea akiba umekua mkubwa.

Tunaposema ‘Staa wa Mchezo’ ni wananchi ambao wamejiajiri kupitia sekta ya kilimo, ufugaji, uvuvi, madini (wachimbaji wadogo wadogo), usafirishaji (boda boda na bajaji), sekta ya biashara ndogo ndogo (Machinga, Mama/Baba lishe, ususi, muuza mkaa, muuza nyanya na staa wengine wote). Ujio wa ‘Hifadhi Scheme’ unatoa nafasi kwa NSSF kushika usukani na kuwa staa wa mchezo katika maisha ya uzeeni au pindi majanga yanapotokea kwa wananchi waliojiajiri ambapo NSSF inakuhakikishia inalinda kesho yako kwa kutoa huduma na mafao mbalimbali kwa mujibu wa sheria. Kujiunga na kuchangia ni rahisi tu kwa kubofya *152*00# ambapo mwanachama anaweza kuchangia shilingi 30,000 au zaidi kwa kutoa kidogo kidogo kwa siku bukubuku, wiki, mwezi au msimu kulingana na kipato chake na kunufaika na mafao yote yanayotolewa na NSSF yakiwemo ya matibabu.

NSSF STAA WA MCHEZO, HIFADHI SCHEME – HIFADHI YA JAMII KWA WOTE











DC MAFIA AZINDUA UVUNAJI WA JONGOO

Mkuu wa Wilaya ya Mafia, Mhe. Aziza Mangosongo amezindua uvunaji wa jongoo bahari katika kitalu kilichopo kijiji cha Dongo, kitongoji cha Mfuruni Julai 30, 2024.

Uvunaji huo wa jongoo bahari umezinduliwa rasmi kwa mara ya kwanza ambapo Mhe. Mangosongo amempongeza mfugaji wa jongoo bahari, mzee Mpogo kwa mchango wake wa kendeleza uchumi wa buluu pamoja na kuleta fursa ya ajira kwa vijana.

" Tumevutiwa sana, vijana wengi wangepatiwa elimu na kujishughulisha na ufugaji wa jongoo bahari, basi wangejikwamua na tatizo la ajira. Kwa upande mwengine, mradi huu unatunza mazingira na ndivyo ambavyo viongozi wetu, hasa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anavyotutaka kujikita katika uchumi wa buluu na kutunza mazingira" alisema Mhe. Mangosongo.

Kwa upande wake, Mfugaji wa jongoo bahari Mzee Waziri Mpogo, ameipongeza Serikali kupitia Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na Halmashauri kwa kutoa ushirikiano kuwezesha fursa hiyo kuwepo pamoja na kuwaomba wakazi wa Mafia wajitokeze kufanya shughuli hiyo ili kuifungua wilaya zaidi kwenye suala la uchumi wa buluu.

Lengo langu ni kutaka wafugaji wadogo wadogo waweze kupata mbegu hapahapa Wilayani badala ya kuzifuata Bagamoyo ama sehemu nyingine" alisema Mzee Mpogo. Nimepata faraja pia kuona mazingira yapo salama kwa sababu mradi huu unasaidia kutunza mazingira, hivyo nawaomba viongozi na wananchi wote tushirikiane katika kukuza uchumi wa buluu" aliongeza.

Mradi huo uliogharimu Shilingi Milioni 176, umekuwa msaada kwa vijana kwa kuwasaidia kuwapa fursa ya ajira.

" Nawaomba vijana wenzangu kujitokeza katika mradi huu badala ya kujishughulisha na mambo ya uhalifu, tunaweza pia kuunda kikundi chetu na kujikwamua kiuchumi" alisema Salum Alawi, kijana anayefanya kazi katika kampuni ya Mpogo Ocean Ranching inayojihusisha na ufugaji wa jongoo bahari.

 

Mbunge wa Chalinze ameshiriki kikao cha Baraza la Madiwani Cha Chama Cha Mapinduzi kuchagua Diwani

 Mbunge wa Chalinze,Ridhiwani Kikwete ameshiriki kikao cha Baraza la Madiwani Cha Chama Cha Mapinduzi kuchagua diwani atakayegombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Chalinze kilichofanyika Chalinze ,mapema leo.#KaziInaendelea




 

MA DC WAJENGEWA UWEZO KUSIMAMIA UTOAJI WA MIKOPO YA ASILIMIA 10


 

Na. James Mwanamyoto, OR-TAMISEMI 

 

Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais - TAMISEMI Bw. Sospeter Mtwale amesema Wakuu wa Wilaya wanapatiwa mafunzo na Ofisi ya Rais -TAMISEMI ya kuwajengea uwezo wa kusimamia zoezi la utoaji na urejeshaji wa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri za Wilaya kwa akina mama, vijana na wenye ulemavu. 

 

Bw. Mtwale amesema hayo leo katika Ukumbi wa Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere Kibaha mkoani Pwani kwa Niaba ya Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais - TAMISEMI Bw. Adolf Ndunguru wakati akifungua kikao kazi cha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa na Wakuu wa Wilaya zote nchini 

 

Bw. Mtwale amesema, Serikali imeanza kutoa mikopo ya asilimia 10 baada ya hapo awali kusitishwa kutokana na changamoto jilizojitokeza, na kuongeza kuwa Ofisi ya Rais – TAMISEMI imeshapitia kanuni na kufanya maboresho na ikaona ni vema Wakuu wa Wilaya wakapitishwa katika kanuni hizo ili waweze kushiriki kikamilifu katika usimamizi wa utoaji wa mikopo hiyo. 

 

Tumeona ni vema nanyi mkapitishwa katika kanuni hizo ili tuwe na uelewa wa pamoja katika kusimamia utoaji wa mikopo hiyo ili mikopo hiyo iwe na tija kwa watakaonufaika na katika taifa kwa ujumla, Bw. Mtwale amesisitiza. 

 

Sanjali na hilo, Bw. Mtwale amesema Wakuu wa Wilaya  watapitishwa katika taarifa ya ukaguzi ya mwaka wa fedha 2022/23 ili wafahamu hoja zilizoibuliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwani nao ni wasimamizi wa halmashauri zilizopo katika maeneo yao ya utawala 

 

Ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya Wakuu wa Wilaya nchini, Bw. Mtwale amesema Ofisi ya Rais - TAMISEMI imemualika mtaalamu wa afya ya akili kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Dkt. Garvin Kweka ili kuwapatia elimu ya afya ya akili na ya namna bora ya kuepukana na magonjwa ya afya ya akili. 

 

Akiwasilisha mada kuhusiana na afya ya akili, mtaalamu wa afya ya akili kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Dkt. Garvin Kweka amewataka Wakuu wa Wilaya kuzingatia mahusiano ya kijamii ili kujenga afya nzuri ya akili itakayowawezesha kutekeleza kikamilifu majukumu yao kwa ufanisi 

 

Mtu anayeenda kwenye jumuiya, vikoba, kanisani au msikitini akipata msiba, msiba wake hauwi sawa na mtu anayejifungia ndani hivyo mahusiano ya kijamii ni lazima yazingatiwe na kisingi ndio utulivu wa afya ya akili,” Dkt. Kweka amesisitiza. 

 

Kikao kazi hicho cha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa na Wakuu wa Wilaya zote nchini, chenye lengo la kuwajengea uwezo kiutendaji viongozi hao kinafanyika kwa siku mbili katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere iliyopo Kibaha mkoani Pwani.



 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Pwani Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa