MTUHUMIWA WA UBAKAJI ATIWA MBARONI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

JESHI la Polisi mkoani Pwani limefanikiwa kumkamata Michael William maarufu (Michael dada), mkazi wa Kiluvya, wilayani Kisarawe anayetuhumiwa kuhusika na matukio ya ubakaji wa vikongwe mkoani hapa.
Akizungumza na waandishi wa habari Kamanda wa polisi mkoa wa Pwani Ulrich Matei alisema jeshi hilo lilikuwa likimsaka mtuhumiwa huyo kwa kipindi kirefu kutokana na kudaiwa kutenda makosa mbalimbali ya ubakaji wa vikongwe na wanawake na kutokomea kusikojulikana.
Alisema, William alitiwa mbaroni juzi baada ya kudaiwa kuhusika katika tukio la wizi wa mifugo lililotokea wiki mbili zilizopita huko Kiluvya.
Pia kamanda Matei alisema, mtuhumiwa huyo anadaiwa kuhusika katika matukio ya ubakaji zaidi ya 10 ambapo kabla ya kufanya vitendo hivyo alikuwa akiwatishia wahusika kwa mapanga.
“Huyu kijana anayejiita Michael dada ni maarufu kwa matukio ya ubakaji na alilisumbua jeshi letu mara kadhaa kwa kunasua mitego aliyowekewa leo tumelazimika kumleta mbele yenu waandishi ili mumuone ni mdogo lakini ametusumbua sana,” alisema.
William alikiri mbele ya waandishi wa habari kuwa miaka ya hivi karibuni aliwahi kufanya unyang’anyi wa kutumia silaha kosa ambalo lilimsababishia kuhukumiwa miaka 30 jela.
Matei alisema kabla kifungo hicho hakijamalizika mwaka 2011 na 2012, William alikata rufaa na kutolewa ili kuendelea na taratibu nyingine na tangu hapo hakuonekana hadi polisi walipofanikiwa kumkamata kwa kosa la wizi wa mifugo.
Hata hivyo William alikana kuhusika na tuhuma zinazomkabili na kudai yeye sio Michael dada kama anavyoitwa bali ni Michael William na tuhuma za ubakaji ni za kusingiziwa.
Chanzo:Tanzania Daima

TAMISEMI:HATUJAAGIZA WATUMISHI KUKATWA MISHAHARA KWA AJILI YA MAABARA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.


Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi-Elimu), Kassimu Majaliwa (pichani), amesema serikali haijaagiza wakurugenzi kukata mishahara kwa watumishi kwa ajili ya ujenzi wa maabara nchini.

Akizungumza juzi wakati wa kukabidhi majengo yaliyojengwa na Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (Wama) katika Shule ya Sekondari Nyamisati, wilayani Rufiji, mkoani Pwani, alisema michango hiyo ni hiyari na siyo lazima.

“Haizuiliwi watumishi kuchangia miradi ya maendeleo, ni wajibu wa viongozi husika kuwaomba, serikali haijawatuma Wakurugenzi kuwakata watumishi mishahara yao kwa ajili ya ujenzi wa maabara,” alifafanua.

Ufafanuzi wa Waziri huyo umekuja wiki chache baada ya NIPASHE kuibua suala la Waratibu Elimu kata na Watendaji, kutakiwa kukusanya michango kutoka kwa walimu huku ikiweka bayana viwango kulingana na ngazi ya mashahara.

Mkoani Tanga, baadhi ya Halmashari nyingine wakuu wa idara wanatakiwa kutoa bati mbili na Sh. 25,000 kila mmoja na watumishi wengine wakiwekewa viwango tofauti tofauti.

Mkoani Kilimanjaro, wazazi wenye watoto wa kidato cha kwanza wanachangia 30,000 na kidato cha pili hadi sita kiasi cha Sh. 20,000 na wakuu wa shule wamepewa barua za maelekezo kutoka kwa wakurugenzi wa halmashauri.

Kwa mujibu wa barua ya Septemba 15, mwaka huu, kutoka moja ya Halmashauri nchini (jina limehifadhiwa) kwenda kwa waratibu wa elimu wa kata, ikiwa na kichwa cha habari cha Michango ya maendeleo kuchangia ujenzi wa maabara, imewataka waratibu hao kukusanya fedha hizo kutoka kwa walimu.

Aidha, barua hiyo ambayo NIPASHE imeiona nakala yake, imeeleza kuwa kulingana na agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania juu ya ukamilishwaji wa maabara katika shule zote za sekondari nchini, uongozi wa halmashauri umeridhia uchangiaji huo.

“Kwa barua hii naagiza uchangiaji wa ujenzi wa maabara kutokana na maamuzi ya wilaya,” ilifafanua barua hiyo.

Barua hiyo ilifafanua viwango vya uchangiaji kuwa ni waratibu elimu kata Sh 60,000, walimu ngazi ya mshahara TGTS F-G Sh 60,000, ngazi ya mshahara TGTS D-E Sh 30,000 na TGTS B-C Sh. 20,000.

Aidha, barua hiyo ilieleza kuwa michango hiyo itatolewa kwa awamu mbili Septemba na Oktoba, mwaka huu.
 
CHANZO: NIPASHE

MAJINA YA AWALI YATAJWA KARIBU FESTIVAL ; MWANANCHI COMMUNICATIONS LTD YADHAMINI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Wiki hii, Kampuni ya Mwananchi COMMUNICATIONS Ltd, inayochapisha magazeti ya Mwananchi, Mwanaspoti na The Citizen, imejitosa kudhamini tamasha la kwanza kubwa la sanaa litakalofanyika Bagamoyo Pwani, linalojulikana kwa jina la Karibu Arts and Music Festival.
Kadri siku zinavyozidi kusonga mbele, wasanii wengi wamekuwa wakiomba kushiriki tamasha hilo linalotarajiwa kufanyika Novemba 7 hadi  9 mjini Bagamoyo, ambapo jana orodha ya kwanza ya wasanii waliokidhi vigezo vya kushiriki tamasha hilo imetolewa.
Akizungumza Dar es Salaam jana, meneja wa tamasha hilo, Richard Lupia (Pichani), alisema kuwa wanatarajia wasanii wengi zaidi watajitokeza kushiriki Karibu Arts and Music Festival.
Alisema kuwa tamasha hilo limeanzishwa mwaka huu ambapo linatarajia kushirikisha wasanii mbalimbali  wa ndani na nje ya nchi.
Lupia alisema kuwa hadi sasa idadi ya walioomba kushiriki inaonyesha dhahiri kuwa watakuwa  wasanii wengi ingawa mwaka huu ni mara ya kwanza tamasha hilo kufanyika.
Alisema kuwa wameandaa tamasha hilo kwa lengo la kukuza utamaduni na utalii nchini kwa manufaa ya Watanzania wote.
Alitaja wasanii wa kimataifa waliothibitisha kushiriki kuwa ni pamoja na Panda(Japan), Maria Kate(Ufaransa), IFE Pianki(Uganda), Masayo(Japan), Fantuzz(Marekani), Shiwe Musique(Comoro), Dwmbede(Kenya) na Mbiye Ebrima(Guinea).
Makundi kutoka Tanzania ni pamoja na Jhikoman & Afrikabisa Band, Wahapahapa, Segere Original, Barnaba, Vitalis Maembe, The Spirit Band, Mama Africa, Chibite Zawose, Afrikwetu, Tongwa Ensemble na Leo Mkanyia & Swahili Blues.
Wengine ni Cocodo Band, Hokororo Band, Lumumba Theater, Mswanu Gogo Vibes, Swahili Vibes, Fimbo Band, Abeneko Music, Man Kifimbo, Saganda na Msafiri Zawose.
“Lengo kuu la tamasha ni kusisitiza kurasimishwa kwa tasnia ya muziki  na kuwa na umakini zaidi, lakini kingine ni kukuza uchumi wa eneo husika la Bagamoyo ambalo ni la kihistoria na kuhakikisha sanaa ya asili ya Mtanzania inaonekana katika jukwaa la kimataifa,”alisema Lupia.
Tofauti na matamasha mengine yaliyowahi kufanyika Tanzania Bara, Karibu Arts and Music Festival litatoa burudani kutumia ala kwa asilimia mia moja. Wasanii wote watakaoshiriki, watalazimika kupiga muziki kutumia ala na kuimba na siyo ‘Playback’.
Lupia alisema mbali na kutoa burudani, wasanii pia watapata nafasi ya kujifunza jinsi ya kuunadi muziki wao duniani kwa njia mbalimbali kwa kushiriki warsha zitakazoendeshwa na wataalamu tofauti kutoka pande zote za dunia
Chanzo:Mwananchi

WAFUGAJI WAPINGA KIJIJI CHAO KUBADILISHWA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

WAKAZI wa Kijiji cha Chamakweza Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani, ambao wengi wao ni wafugaji wameweka kambi kwa muda usiojulikana wakipinga kijiji chao kuingizwa kwenye mipango mji.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, walisema Kijiji chao kilitengwa kuwa cha wafugaji tangu mwaka 1974, hivyo endapo kitaingizwa kwenye mipango miji itawalizimu kufuga kisasa jambo ambalo ni gumu kwao.
Kijiji hicho ambacho kina wakazi zaidi ya 4,500 wakiwa na ng’ombe 22,000, mbuzi 6,000 na kondoo 4,000, mipango miji ikianza wakazi wake watalazimika kufuga ng’ombe wasiozidi 10 kila mmoja.
Mwenyekiti mstaafu wa kijiji hicho, Mbambile Kisanjo, alisema wameweka kambi kwa muda usiojulikana kupinga utaratibu wa mipango miji, ambao hawajashirikishwa na viongozi wa serikali wakati mikakati hiyo ikifanyika.
Samwel Mganga, alisema kuwa serikali ya awamu ya kwanza ndiyo iliyowapatia eneo hilo kwa ajili ya wafugaji, hivyo huo utaratibu mpya unaotaka kuanza hawakubaliani nao kwani ni wa kuwahangaisha kwa kuanza kuhama hama.
Nae Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Mkoa wa Pwani, Mohamed Leboi, alisema kuwa anaunga mkono pingamizi linalowekwa na wakazi wa Kijiji hicho kuingizwa kwenye mipango miji kwani litaathiri maendeleo yao na kuharibu mipango waliyojiwekea.
Alivitaja vijiji vilivyotengwa kwa ajili ya wafugaji ambavyo vitakumbwa na adha hiyo kuwa ni pamoja na Lulenge, Ubena, Pera, Malivundo, Chamakweza na Bwilingu ambazo ni sawa na hekta 53,106.
Mwenyekiti wa Kijiji hicho Mikalain Lemwes, alisema kuwa mipango miji wanaihitaji kwa maendeleo, isipokuwa itakapoingia matumizi ya ardhi yatabadilika kutoka eneo la wafugaji na kuwa mji.
Diwani wa kata hiyo ambae ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Bagamoyo, Shukuru Mbato, alipoulizwa kuhusiana na malalamiko hayo, alisema atafanya mkutano na wakazi hao kuzungumzia suala hilo huku akikwepa kueleza ukweli kuhusiana na Kijiji hicho kuingizwa kwenye mipango miji.
chanzo:Tanzania Daima

BASI LA MACHAME SAFARI LANUSURIKA KUPATA AJALI BAADA YA KUHAMA BARABARA




 Picha na Pwani yetu Blog/ Blogs za Mikoa

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

SEKONDARI YA LUGOBA YAJITAJI MIL. 9/-

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

SHULE ya Sekondari Lugoba wilayani hapa Mkoa wa Pwani, inahitaji sh milioni tisa kwa ajili ya ununuzi wa mashine ijulikanayo kama ‘Embozer’ kwa ajili ya kuchapishia mitihani ya wanafunzi wasioona.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa shule hiyo, Abdallah Sakasa, wakati wa mahafali ya 23 ya kidato cha nne, ambako alibainisha endapo mashine hiyo itapatikana, itapunguza gharama zinazotumika kwa sasa.
Sakasa, alisema mashine hiyo ambayo inapatikana Nairobi Kenya,  itatumika kama ‘printer’ ikiunganishwa kwenye kompyuta na kutoa herufi nundu zinazotumiwa na wanafunzi hao.
“Changamoto hii ya upatikanaji wa mashine ya kuchapia hurufi nundu bado ni kubwa katika shule yetu, kwani mashine moja inauzwa sh milioni 1.8 na sisi tuna upungufu wa mashine tano,” alisema.
Aidha, aliainisha changamoto nyingine kuwa ni pamoja na gharama za kemikali na vifaa vya maabara, kutokana na kuwepo kwa wanafunzi wengi wanaosoma masomo ya sayansi katika shule hiyo.
Shule hiyo ambayo ilianzishwa mwaka 1989, sasa ina wanafunzi 1,367 wasichana wakiwa 674 kidato cha kwanza hadi cha sita, ambako wahitimu wa kidato cha nne mwaka huu wakiwa 151.
Chanzo;Tanzania Daima

RC MAHIZA AHIMIZA CHANJO YA SURUA NA RUBELLA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

MKUU wa Mkoa wa Pwani, Mwantum Mahiza, amewataka wananchi kushiriki kikamilifu kwenye zoezi la chanjo ya surua na rubella inayoanza leo hadi Oktoba 24 mwaka huu na kwamba hazina madhara.
Mahiza, alitoa wito huo wakati akizungumza na waandishi wa habari pamoja na viongozi wa Mkoa kuhusiana na zoezi hilo, alisema viongozi wa ngazi zote mkoani hapa, wanatakiwa kushiriki kikamilifu kuhamasisha wananchi kujitokeza kwenye vituo vilivyopangwa.
“Viongozi wa serikali za mitaa na viongozi wa ngazi zote pamoja na wa madhehebu yote, tuwahamasishe wananchi wajitokeze, dawa hizi hazina madhara yoyote na chanjo hizi ni kinga kwa magonjwa mengine,” alisema Mahiza.
Aidha, alisema zoezi hilo litaambatana na utoaji wa dawa za matende na mabusha, chanjo ya surua rubella, matone ya vitamin A na dawa za minyoo.
Awali akitoa taarifa kuhusiana na zoezi hilo, Mratibu wa chanjo ya watoto mkoani Pwani, Abbas Hincha, alisema chanjo ya surua na rubella walengwa ni 458,000 vitamin A 390,000 matende na mabusha 850,000.
Chanzo:Tanzania Daima

WAKUU WA IDARA WASIKIMBIE WANANCHI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

WAKUU wa Idara katika Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani, wametakiwa kuachana na utaratibu wa kutuma wawakilishi kwenye mikutano ya wananchi kwani kufanya hivyo ni kuibua hofu ya maendeleo kwa wananchi.
Baadhi ya wakuu wa idara, wamekuwa wakituma wawakilishi mara kwa mara katika mikutano na hivyo wananchi kukosa majibu ya moja kwa moja kutoka kwa viongozi wao wa serikali.
Wito huo umetolewa hivi karibuni na Mbunge wa Kisarawe, Selemani Jafo, wakati akizungumza na wakazi wa kitongoji cha Masimba, ambako alisema kuwa uwakilishi huo umekuwa ukimkera kwani unasababisha wananchi kukosa imani na viongozi waliopo madarakani.
Alisema kitendo cha baadhi ya wakuu wa idara kutuma wawakilishi, kimekuwa kikisababisha hofu ya maendeleo kwa wananchi hasa kwenye utekelezaji wa miradi mbalimbali, kwa kukosa takwimu na kushindwa kujibu namna ya utatuzi wa changamoto.
“Nakushukuru Ofsa Elimu wa Wilaya kwa maana kila ninapokupa taarifa ya kushiriki na mimi kwenye mikutano amekuwa akifanya hivyo na kusaidia kutoa majibu ya moja kwa moja kwa maswali ya wananchi, uwakilishi kwa baadhi ya watendaji umekuwa kikwazo cha maendeleo ambacho naendelea kupiga vita tabia hii inayoleta hofu kwa wananchi,” alisema Jafo.


Hivi karibuni ujenzi wa nyumba ya mwalimu katika kitongoji cha Masimba ulikwama kwa zaidi ya miezi sita kutokana na wakandarasi kuhitaji fedha kubwa tofauti na iliyotengwa na Halmashauri.
Chanzo;Tanzania Daima

RC: TAKWIMU ZA SENSA ZITUMIKE KUPANGA MIPANGO YA MAENDELEO

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani,Mwatumu Mahiza.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mwatumu Mahiza amewataka wananchi pamoja na watumishi wa mikoa, wilaya na Halmashauri nchini kutumia takwimu za sensa ya watu na makazi ya  mwaka 2012 kupanga mipango ya kuziletea maendeleo.

Mahiza aliyasema hayo katika semina ya usambazaji wa matokeo ya sensa ya watu na makazi katika mkoa huo  ambayo ilizinduliwa ramsi jana katika ofisi za mkoa wa mkoa wa Pwani mjini Kibaha.

Alisema endapo takwimu hizo zitatumika ipasavyo na kwa usahihi zitasaidia kwa kiwango kikubwa kuleta maendeleo kwa wananchi na nchi nzima kwa ujumla.

“Serikali iliandaa sensa hii kwa lengo la kupata takwimubora zitakazotumika katika kupanga, kutunga sera, kutathmini utekelezaji wa mipango ya maendeleo na utoaji huduma kwa wananchi ili kuchangia kiwango cha maisha cha kila mwananchi,” alisema na kuongeza:

“Kwa kutumia takwimu hizi  ni lazima itawasaidia  kupanga mipango yenu vizuri kulingana na idadi ya watu mlionao katika familia, kijiji, halmashauri au katika mikoa yenu, siyo rahisi wewe una familia kubwa halafu ukapika ugali kidogo ni lazima utapika kulingana na ukubwa wa familia, vivyo hivyo katika halmashauri au mikoa mipango mtakayopanga ni lazima mhakikishe inaendana na idadi ya watu mlionao.”

Aidha, aliitaka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kuanzisha chombo maalum kitakachotumika kudhibiti matumizi na utoaji ovyo wa takwimu zisizo sahihi ambazo zimekuwa zikitolewa na watu mbalimbali na taasisi mbalimbali.

“Ipo haja ya NBS kuanzisha chombo cha Information data control ambacho kitadhibiti matumizi holela ya takwimu, tofauti na ilivyo sasa mtu akiamua kutoa takwimu anatoa hata bila ya kudhibitishwa na chombo husika, hiyo itasaidia, sisi tunafahamu kuwa TBS wa  takwimu ni NBS, hivyo tunahitaji kila takwimu zinazotolewa ziwe zimethibitishwa na chombo hicho,” alisema Mahiza.

Mkurugenzi Mkuu wa NBS, Dk. Albina Chuwa, alisema usambazaji wa matokeo ya sensa hiyo unatarajiwa kuanza kusambazwa hivi karibuni katika mikoa yote nchini, katika wilaya, mikoa na hata vijiji.

Naye Mwakilishi wa Shirika la Idadi ya watu na Makazi Duniani (UNFPA), DK. Collins Opiyo, aliwataka vijana kutumia takwimu hizo katika kutimiza ndoto zao.
 
SOURCE: NIPASHE

WAGONJWA WA AKILI WALALA WODI MOJA NA WENGINE

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.


Hospitali kongwe ya Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani, inakabiliwa na upungufu wa wodi za kulaza wagonjwa na kulazimika kuwachanganya wagonjwa wenye matatizo ya akili na wale wenye  maradhi mengine.

Muuguzi wa hospitali hiyo, Bahati Kuguru, alisema hospitali hiyo ni miongoni mwa zile zinazofanya kazi katika mazingira magumu hasa ya kutokuwa na wodi maalum za kulaza wagonjwa hali inayohatarisha usalama wa wagonjwa na wauguzi.

 “Serikali iangalie namna ya kunusuru hali hii haraka iwezekanavyo kwa sababu wagonjwa wenye matatizo ya akili kitabibu wanahitaji kulazwa wodi maalum peke yao, vinginevyo wanaweza kuleta madhara kwa wagonjwa wengine na wauguzi pia,” alisema Kuguru.

Pia alisema chumba cha kuhifadhia wagonjwa  cha hospitali hiyo ni kidogo na hakina majokofu jambo linalosababisha ndugu kulazimishwa kuchukua miili ya ndugu zao muda mfupi baada ya kufariki dunia.

Aliongeza kuwa ingawa serikali inazitambua changamoto zilizoko, bado haijashirikiana na hospitali hiyo katika kuboresha mazingira halisi badala yake miundombinu yake inazidi kuchakaa.

“Tunaomba serikali ichukue maamuzi magumu katika kutatua suala hili, kwanza itupatie gari ya usafiri itakayotumika kutoa huduma ndani na nje ya hospitali pale inapobidi pamoja na kujenga majengo yatakayojitegemea kutokana na tatizo la wagonjwa,” alisema Kaguru.

Mgonjwa wa matatizo ya akili aliyelazwa katika wodi ya wananwake katika hospitali hiyo, Roida Mwangaya, alisema serikali iboreshe hospitali hiyo kwa sababu ni kitovu cha wakazi wa ndani na nje ya eneo hilo.

“Ipatikane wodi  maalumu za kulaza wanawake, watoto, wanaume pamoja na kitengo maalum cha kuwalaza na kuwalea wagonjwa wa matatizo ya akili,” alisema Mwangaya.
 
CHANZO: NIPASHE

PSPF YATOA MSAADA WA KOMPYUTA 12 KWA VYUO VIWILI BAGAMOYO

 Afisa Mahusiano wa PSPF Coleta Mnyamani kushoto Akimkabidhi Msaada wa Kompyuta Mkuu wa Chuo Kikuu teule cha Marian Father Luke Mbefo  ambapo Kompyuta hizo zitatumika katika Kuhifadhi Nyaraka mbalimbali za Maktaba
 
 Mkuu wa Chuo Kikuu teule cha Marian Father Luke Mbefo  kulia akimshukuru Afisa Mahusiano wa PSPF Bi. Coleta Mnyamani kwa msaada huo
 Mwakirishi wa Shirika la Roho Mtakatifu Father Nicetas Kyara akitoa neno la Shukurani Baada ya kukabidhiwa msaada wa Kompyuta Mbili za kisasa kutoka Mfuko wa Pensheni wa PSPF
 Afisa Mahusiano wa PSPF Bi. Coleta Mnyamani akizungumza neno Baada ya kukabidhi Msaada huo
Afisa wa Fedha kutoka PSPF Bwana Samwel Haule Akizungumza Jambo wakati wa Makabidhiano wa Kompyuta hizo katika Chuo Kikuu teule cha Marian
 Mkuu wa Chuo teule cha Marian Father Luke Mbefo wakiteta Jambo na Afisa Mahusiano wa Pspf Bi Coleta Haule Baada ya Kukabidhi Msaada huo
 Picha ya Pamoja ya Viongozi wa PSPF na Chuo  Kikuu teule cha Marian
Kulia ni Meneja wa Pwani wa PSPF Msafiri S. Mugaka akimkabidhi Kompyuta 10 Mwenyekiti wa Baraza la Chuo cha Ukutubi,Uhifadhi wa Kumbukumbu na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania Dkt. Ally S. Mcharazo kwa niaba ya chuo hicho
Meneja wa Pwani wa PSPF Msafiri S. Mugaka  akizungumza na wanafunzi wa Chuo cha Ukutubi,Uhifadhi wa Kumbukumbu pamoja na wagani waalikwa wakati wa kukabidhi msaada huo wa kompyuta 10 za kisasa
Rais wa Chuo cha Chuo cha Ukutubi,Uhifadhi wa Kumbukumbu Daudi Joho akitoa neno la Asante Baadhi ya Kukabidhiwa Msaada huo 
Mbele ni Maofisa wa Mfuko wa Pensheni wa PSPF
Mwenyekiti wa Baraza la Chuo cha Ukutubi,Uhifadhi wa Kumbukumbu na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania Dkt. Ally S. Mcharazo  akitoa neno la Shukurani
 Baadhi ya wanafunzi wakisoma Vipeperushi vya PSPF
Wanafunzi wakiwa wanafuatilia kwa makini
Kila mtu anachukua Kumbukumbu


Mfuko wa pensheni wa PSPF waendelea kukuza elimu ya Tehama katika vyuo mbalimbali hapa nchini kwa kutoa msaada wa jumla ya kompyuta 12 katika chuo cha Ukutubi Uhifadhi wa Nyaraka Bagamoyo na chuo Teule  ambacho kitakuwa kikiendeshwa chini ya saint augustine's university  (SAUTI) ambapo  kompyuta kumi (10) zimetolewa  katika chuo cha Ukutubi Uhifadhi wa Nyaraka na Mbili zimetolewa katika chuo teule cha cha Mariana university College vyote vilivyopo bagamoyo katika mkoa wa pwani.

Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo afisa mahusiano wa PSPF Bi. Coletha Mnyamani amesema zoezi hilo limeanza lakin halitaishia hapo kwani ni zoezi endelevu kwani wameamua kusaidia jamii hususani kwa wanafunzi ilikuweza kuwajengea ujuzi katika masomo yao pamoja na kutunza nyaraka zao kisasa na sio katika makaratasi  kama ilivyo kuwa hapo zamani

Kwaupande wake Meneja wa  Wa PSPF Mkoa wa Pwani  Bw.Msafiri S Mugaka amesema kuwa wameweza kutimiza ahadi waliyo ahidi kwa chuo cha Ukutubi Uhifadhi wa Nyaraka na kuweza kutoa msaada kwa chuo teule cha Mariana university College Hivyo wawaomba wananchi kuiamini na kuendelea kuwa wanafamilia wa mfuko huo wa pensheni

Naye Mwenyekiti wa Baraza la chuo cha Ukutubi Uhifadhi wa Nyaraka na mkurugenzi wa wa Bodi ya Huduma za Maktaba –Tanzania Ally  Mcharazo kilichopo Bagamoyo wakati akipokea msaada huo kutoka kwa maafisa wa mfuko wa PSPF makao makuu Dar es saalam Amesea wanatoa shukrani kwa Mfuko huo kwani umeweza kuwasogeza katika huduma za kisasa kwa kuwapelekea kompyuta hizo nyaraka zote zitakuwa zikitunzwa katika hali iliyo salama na sio katika hali ya kizamani na kazi kuenda kwa haraka zaidi kwani kompyuta husaidia katika kuokoa muda kazini.

Pia Bw.Samweli Haule ambaye ni afisa Wa Fedha Wa Mfuko Wa Pensheni wa PSPF Aliweza kutoa maneno ya kuwaasa wanafunzi kwa kuwa makini na wao hawata choka kutoa msaada pindi wanapo kuwa wamekwama ili kuweza kuwaweka wanafunzi wote katika hali ya kisasa zaidi

Mkuu wa Chuo cha Mariana university College Father Luke Mbefo pia naye aliweza kushukuru Mfuko wa PSPF kwa kuona umuhimu wa kuweza kusaidia upande wa elimu kwa kuchangia kwa aina mbalimbali bila kuchoka na kuchagua rangi wala dini

Hivyo Mfuko wa Pensheni PSPF Umetoa wito kwa wananchi  pamoja na vyuo mbalimbali kwakuwa wao wapo kwamoyo kwaajili ya wananchi na kuhakikisha kuweza kuikomboa elimu yetu kwa kuipelekea wepesi zaidi katika hali ya udigitali kuachana na analogia,kwani huop ni mwanzo tu mambo mengine yatafuata tena mazuri kutoka PSPF


VIONGOZI WATAKIWA KUTOPUUZA TAASISI ZA DINI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

VIONGOZI wa Serikali, wametakiwa kutopuuza mialiko kutoka Taasisi za kidini kwani katika shughuli hizo za kijamii hutumika kufikisha changamoto zao ambazo zinahitaji ufumbuzi.
Ombi hilo limetolewa mjini Kibaha juzi, wakati wa sherehe za Baraza la Idd zilizofanyika katika Taasisi ya kidini inayojishughulisha na kutoa huduma ya elimu na kusaidia makundi mbalimbali ya WIPHAS, na Mwenyekiti wa maandalizi ya baraza hilo, Mohamed Kiaratu.
Kiaratu, aliwaambia waandishi wa habari kuwa, viongozi wa serikali ni muhimu kushirikiana na wananchi hasa pale wanapopewa mialiko, kwani wao wana ufafanuzi wa mambo mbalimbali ambayo ni changamoto kwenye Taasisi.
“Viongozi wa serikali wanatakiwa wasitupuuze, wanapopata mialiko yetu wajitahidi kushiriki pamoja na sisi, kwani tuna mambo mengi ya kuwakilisha kwao ambayo tunaamini wao ndio wenye ufafanuzi wa kina,” alisema Kiaratu.
Akizungumzia suala la ujenzi wa ofisi ya Bakwata Mkoa wa Pwani, aliwaomba wadau mbalimbali kuchangia ili kufanikisha lengo hilo, ambako hadi sasa ujenzi huo umegharimu sh milioni 200 huku ikihitajika milioni 300 kukamilisha.
Akihutumia mamia ya wakazi wa Kibaha waliohudhuria baraza hilo, Mbunge wa Mafia, Abdukarim Shaha, alitoa wito kwa Taasisi hiyo kutafuta namna ya kufungua vituo vingine ili huduma wanayoitoa ifikie katika mikoa mingine ya jirani.
Chanzo:Tanzania Daima

MADIWANI KYELA WAJINOA USAFI WA MAZINGIRA KIBAHA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

MADIWANI wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyela mkoani Mbeya wamefanya ziara ya mafunzo kwa kuitembelea Halmashauri ya Mji Kibaha kwa lengo la kujifunza jinsi ya uboreshaji na usafi wa mazingira.
Akizungumza katika kikao cha mafunzo hayo yaliyofanyika ukumbi wa Halmashauri ya Mji Kibaha yakiwakutanisha Madiwani na wakuu wa idara kwa nia ya kupeana maarifa, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kyela, Gabriel Kipija, alisema hawakuja Kibaha kimakosa bali kutokana na ukweli wa mambo kuwa, Kibaha ni safi.
Akiwakaribisha, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Kibaha, Sloom Bagumesh, aliwapongeza Madiwani na watendaji kutoka Kyela kwa kuja kujifunza na wamefanya chaguo sahihi, kwani si jambo la kubeza kuwa  miaka ya hivi karibu Kibaha imefanya vema katika nyanja za usafi wa mazingira.
Akisoma taarifa ya namna anavyokabiliana na usafi wa mazingira katika Mji wa Kibaha, Mkuu wa idara hiyo, Tumaini Kayila, alisema pamoja na kufanya mikutano na wananchi kutoa elimu namna ya utunzaji sahihi wa mazingira kuanzia ngazi ya mtaa, vimeundwa vikundi 13 vinavyofanya kazi ya uzoaji taka majumbani.
Aidha, Halmashauri imekuwa ikiwapa vitendea kazi kama matoroli, baiskeli za magurudumu matatu ‘guta’, na pikipiki za magurudumu matatu kwa ajili ya kusafirishia taka kutoka sehemu za pembezoni na kuzikusanya kwenye vizimba.
“…dampo letu lipo nje ya Mji, vikundi hivi hukusanya taka toka sehemu mbalimbali na kuziweke kwenye vizimba. Baada ya hapo magari yetu mawili yenye uwezo wa tani 7 huzisafirisha mpaka dampo ambapo kwa siku tuna uwezo wa kusafirisha tani 14,” alisema.
Mwaka wa fedha 2013/2014, Kibaha imeshika nafasi ya tatu kwa utunzaji na usafi wa mazingira ikiwa nyuma ya Jiji la Mwanza na Manispaa ya Moshi.
Ziara hiyo iliyokuwa na ujumbe wa watu 37 wakiwemo madiwani 27 na watendaji 10 pamoja na mambo mengine, ililenga pia kujifunza namna ya upimaji na uuzaji wa viwanja na ukusanyaji wa mapato kwa njia ya Ki-elektoniki hasa kwa kutumia Max Malipo.
Chanzo:Tanzania Daima

MADINI YA SH15.8 BILIONI YAKAMATWA YAKITOROSHWA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

Wakala wa Ukaguzi wa Madini nchini (TMAA), umekamata madini yenye thamani ya Sh15.8 bilioni yaliyokuwa yakitoroshwa kwenda nje ya nchi bila ya kibali na kukwepa kulipa kodi ya mapato.
Kaimu Mkurugenzi wa Udhibiti wa Uzalishaji na Biashara ya Madini wa TMAA, Conrad Mtui alisema kuwa kiasi hicho cha madini aina mbalimbali kilikamatwa kati ya Julai, 2012 hadi Agosti, mwaka huu.
Mtui aliwaambia waandishi wa habari juzi katika ziara ya kutembelea migodi ya madini ya ujenzi ya Lugoba na Msolwa wilayani Bagamoyo, kuwa wakala ulikamata madini hayo katika matukio 53 ambayo yaliwahusisha mawakala wa madini.
“Baada ya kuanzisha madawati ya ukaguzi kwenye viwanja vya Kimataifa vya Ndege vya Julius Nyerere (JNIA), Kilimanjaro na Mwanza, tuliwakamata wote waliokuwa wakijaribu kusafirisha madini hayo kinyume cha sheria, matukio haya yanaweza pia kuongezeka muda wowote.
“Wahusika wamefikishwa mahakamani na baadhi yao wamehukumiwa na madini yao kutaifishwa kwa mujibu wa Sheria ya Madini ya mwaka 2010,” alisema Mtui.
Alipoulizwa kama kuna wachimbaji wakubwa waliokamatwa wakifanya hujuma hiyo, Mtui alisema waliokamatwa wengi walikuwa wafanyabiashara wadogo na madalali na hakukuwa na kampuni kubwa kwa kuwa kuna utaratibu maalumu wa ukaguzi na usafirishaji.
Hata hivyo, Mtui alisema baada ya kukaza uzi wa ukaguzi walifanikiwa kuongeza mrabaha kutoka kwenye migodi mikubwa ya dhahabu kiasi cha Dola za Marekani 427.98 kuanzia mwaka 2005 hadi mwishoni mwa Agosti mwaka huu.
“Wakala ulifanya ukaguzi na uhakiki wa madini yaliyozalishwa na kuuzwa na migodi mikubwa nchini. Ukaguzi huo ulisaidia kujua kiasi na thamani halisi ya madini yaliyozalishwa na kuuzwa kutoka migodi mbalimbali, ikiwamo saba ya dhahabu ya Geita, Golden Pride, Bulyanhulu, Tulawaka, North Mara, Buzwagi na New Luika,” alisema.
Pamoja na kujinadi kwa mafanikio hayo, Mtui alisema bado kuna ujanja wa utoroshaji kupitia njia za panya na upungufu wa rasilimali watu unawazuia kufanya ukaguzi katika migodi midogo, hivyo kuchangia upotevu wa mapato.
“Tuna wakaguzi wetu katika baadhi ya migodi midogo yenye uzalishaji mkubwa...lakini kwa mingine ni hasara kwa sababu unaweza kukuta malipo ya wakaguzi ni makubwa kuliko mrabaha unaopatikana,” alisema.
Chanzo:mwananchi

MAHIZA AZISHUKIA ASASI ZA UKIMWI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

MKUU wa Mkoa wa Pwani, Mwantum Mahiza, amesema anashangazwa na uwepo wa asasi nyingi zinazotoa elimu namna ya kuepuka maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi huku takwimu za maambukizi zikiendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka.
Amesema anashindwa kuelewa kazi inayofanywa na asasi hizo, kwani bado kuna maambukizi mapya mkoani hapa huku zikiendelea kupata fedha kutoka kwa wafadhili kwa ajili ya kutoa elimu hiyo.
Mahiza, alisema ni wakati sasa kila asasi kuweka wazi kazi inayofanya na maeneo yake ili ufuatiliaji ufanyike, badala ya kuendelea kuwa na mlundikano wa asasi ambazo kazi zinazofanywa taarifa zake hazifiki kwenye Halmashauri.
Aidha, Mahiza alizionya asasi zisizo za serikali zinazowatumia watoto yatima kama sehemu ya kujipatia mitaji kutoka kwa wafadhili, kuacha tabia hiyo na atakayebainika hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
Mkuu huyo wa Mkoa, alitoa kauli hizo kwa nyakati tofauti Mjini Kibaha katika mkutano wa mashirika yasiyo ya kiserikali uliokuwa umeandaliwa chini ya ofisi ya Idara ya Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Pwani, kupitia ofisa wake Asha Itelewe, ambako lengo ilikuwa kujadili changamoto zilizopo.
Mahiza, alisema zipo asasi nyingi ambazo zimekuwa zikitumia watoto yatima kupata fedha kwa wafadhili na wanapofanikiwa, watoto hao wanaachwa wakiendelea na maisha magumu na wao kufanyakazi zenye maslahi yao binafsi.
Alisema kuwa, jambo la msingi ni kuhakikisha wanafanyakazi ya kutafuta fedha, ambazo kwa kiasi kikubwa zitawaelimisha ndugu ili wajue namna ya kuwatunza watoto hao kuliko kufanya mambo ambayo yanadhalilisha binadamu wenzao.
Mkutano huo ulishirikisha asasi kutoka Wilaya za Mkuranga, Rufiji, Kisarawe, Kibaha na Bagamoyo, nyingi zikiwa zimejikita kufanya kazi katika masuala ya ukimwi, yatima, mazingira, jinsia na wazee.

WAKULIMA WALIA NA MIFUGO

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

WAKULIMA kwenye mashamba yaliyopo katika vitongoji vilivyomo ndani ya Kijiji cha Kidogozero, Kata ya Vigwaza Bagamoyo Mkoa wa Pwani wamauomba uongozi mkoani humo kusaidia ili kuondokana na kero ya mifugo inayoingia kwenye mashamba.

Wakazi Bw.Said Msumi na Ally Mwenda kwa niaba ya wenzao waliwaeleza waandishi wa habari kuwa kero hiyo imekuwa kubwa kiasi cha kuwakatisha tamaa kwenye kuendeleza kilimo.

"Kama mnavyoyaona makundi yamifugo hii ndio hali halisi kila kukicha hali iko hivi,hatuna raha yakuendelea nakilimo kutokana na mifugo kwani imekuwa kero kubwa,tunawaomba viongozi ngazi ya mkoa watusaidie," alisema Msumi.

Aliongeza kwamba,kutokana na ukweli huo unapofika wakati wa kilimo wanalazimika kutumia zaidi ya sh. lakimoja kwa ajili ya kuingiza trekta badala ya sh.50,000 kwa eka hii hiyo inatokana na ardhi kuwa ngumu hatua ambayo wamiliki wa vyombo hivyo kutoza kiasi hicho.

Kwa upande wake Mwenda alisema wachungaji wanaingiza mifugo katika mashamba hali inayotishia usalama kwenye maeneo hayo na jamii hiyo inayojihusisha na mifugo.

" Hii hali inatisha sana hivyo tunawaomba viongozi ngazi ya mkoa wa wafike kutusaidia ili nasi tuwe na uhuru wakutekeleza kilimo chetu ambacho ndio tunachokitegemea katika kuendesha maisha yetu," alisema Bw. Mwenda .

Akizungumzia changamoto hiyo mwenyeki ti wa kijiji hicho Bw.Ally Mmanga amekiri kuwepo kwa hali hiyo nakueleza wamewasiliana na uongozi wa NAFCO uli opojirani kabisa na kijiji ili kusaidia na kudhibiti hali hiyo

TAMASHA KUBWA LA KARIBU MUSIC FESTIVAL KUFANYIKA BAGAMOYO‏



 Meneja wa tamasha la Karibu Music Festival, Richard Lupia akizungumza katika mkutano na waandishi wa Habari Dar es Salaam hii leo juu ya maandalizi ya tamasha hilo.
 Meneja wa tamasha la Karibu Music Festival, Richard Lupia akizungumza katika mkutano na waandishi wa Habari Dar es Salaam hii leo juu ya maandalizi ya tamasha hilo. Kushoto ni Mratibu wa Tamsha, Issam Ramadhan na Kulia ni Afisa Habari wa Karibu Music Festival, Said Hashim.


Meneja wa tamasha la Karibu Music Festival, Richard Lupia akifafanua jambo katika mkutano na waandishi wa Habari Dar es Salaam hii leo juu ya maandalizi ya tamasha hilo. Kushoto ni Mratibu wa Tamsha, Issam Ramadhan
 ********
Na Father Kidevu Blog
Tamasha kubwa la Karibu International Music Festival, linataraji kufanyika nchini kwa mara ya kwanza katika Pwani ya viwanja vya Taasisi ya Sanaa Bagamoyo (TASUBA).

Waratibu wa Tamasha hilo Karibu Cultural Promotions kupitia kwa Meneja wa Onesho hilo, Richard Lupia, amesema litafanyika kwa siku tatu kuanzia Novemba 7-9 Mwaka huu wa 2014.

Lupia amesema vikundi zaidi ya 30 na wasanii zaidi ya 500 kutoka kila kona ya dunia wanaopiga muziki wa dansi,Reggae, Hip Hop, Taarab, Ngoma za Asili, Bongofleva na Ghani wanataraji kushiriki.

“Lengo kuu la Tamasha, pamoja kukazia katika kurasimisha tasnia ya muziki kuwa na umakini zaidi, lakini kingine ni kukuza uchumi wa eneo husika la Bagamoyo ambalo ni la kihistoria, pamoja na kuhakikisha sanaa ya asili ya mtanzania inapata kuonekana katika jukwaa la kimataifa,”alisema Lupia.

Tofauti na matamasha mengine yaliyowahi kufanyika Tanzania Bara, hili
litakuwa likitumia ala kwa asilimia mia moja, wasanii wote watakaoshiriki,
watalazimika kutumia muziki wa ala kuimba na sio Playback.

Ukiachana na burudani, wasanii pia watapata nafasi ya kujifunza jinsi ya
kuunadi muziki wao duniani kwa njia mbali mbali ambako kutakuwa na warsha kutoka kwa wataalamu mbali mbali toka pembe zote za dunia.

Tamasha litakuwa likiendeshwa mchana na usiku ambapo mchana sanaa za michoro, mavazi na kuchonga zitakuwa zikioneshwa eneo la tamasha huku semina na mijadala ya jinsi ya kuupeleka muziki wa tanzania katika hatua nyingine za kimaendeleo zikiwa zinaendelea.

Mpaka sasa zaidi ya vikundi 100 vimeomba kushiriki tamasha kutoka pembe mbali mbali za dunia, tuko katika kuvichuja na kuangalia ubora wao, na Mungu akipenda, wiki ijayo tutakuja tena kuwaambia majina ya wasanii watakaoshiriki tamasha hili linalotarajiwa kuwa kubwa kuliko yote Afrika ya Mashariki.

Lengo la kuja hapa mbele yenu kwa leo lilikuwa ni kuwajulisha kuhusiana na
hili na kutoa rasmi ombi letu kwenu la kusambaza ujumbe kuhusiana na fursa hii kwa wasanii wetu kujifunza kutoka kwa wenzetu, jinsi wenzetu kutoka nchi zinazoendelea, wanavyofaidika na sanaa yao ili na sisi tuweze kujikomboa.

Tunatanguliza shukrani zetu kwa kuhudhuria kwanza, lakini kingine tunaomba ushirikiano, bado sisi ni wachanga, tujitahidi kuhakikisha kwamba muziki wa Tanzania unafika katika kilele cha mafanikio.
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Pwani Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa